Polisi nchi Marekani wanamtafuta mwanamke aliyewaingiza mjini wanajeshi 11 wa Marekani kwa kufunga nao ndoa na kisha kuwaibia mali zao zote waliposafiri na kumuachia nyumba zao.
Mwanamke huyo aliyetajwa kwa jina la Bobbi Ann Finley anaaminika kuwa ni tapeli sugu ambaye amekuwa akiwaingiza mjini wanajeshi wa Marekani kwa takribani miaka 20.
Msako umeanzishwa na polisi kwenye majimbo ya Washington, Nebraska na Texas wakati jeshi la Marekani limemkodisha mpelelezi maalumu kumsaka mwanamke huyo.
Njia yake ya kuwatapeli wanajeshi ni rahisi sana
Hujipeleka kwenye kambi za jeshi la Marekani kuwasaka wanaume waliojaa upweke wa mapenzi ambao wanaandaliwa kwaajili ya kusafirishwa kupelekwa kwenye kambi za Marekani nchini Afghanistan na kwingineko.
Anapofanikiwa kumnasa mwanaume humuongopea kuwa yeye ni binti afisa wa ngazi za juu wa jeshi la Marekani na kwamba ameachiwa urithi mkubwa ambao ataweza kuuchukua iwapo ataolewa.
Baada ya mwanajeshi wa Marekani kuingia mtegoni na kukubali kufunga naye ndoa, Finley huanza maisha ya ndoa na mumewe huyo huku akisubiria kwa hamu siku ambayo mumewe atasafirishwa kwenda nje ya Marekani.
Baada ya mumewe kusafiri, Finley huanza kazi ya kuiba vitu vyote kwenye nyumba na kuzitumia vibaya credit card anazoachiwa. Huhakikisha anawaingiza hasara kubwa kabla ya kutimkia mji mwingine kusaka mwanajeshi mwingine.
Katika miaka yake ya kuwatapeli wanajeshi wa Marekani kuanzia mwaka 1993, Finley amefanikiwa kuwatepeli jumla ya wanajeshi 11 na amezaa watoto tisa na wanajeshi 9 tofauti.
Watoto wake inasemekana wamezagaa katika miji mbalimbali ya Marekani na baadhi yao hawajawahi kuziona sura za baba zao.
Mmojawapo wa wanajeshi aliyelizwa na Finley alikuwa ni Shane Cheeseman, ambaye alikutana na Finley mwaka 1998 kwenye kambi ya jeshi ya Fort Hood mjini Texas.
"Nilifunga naye ndoa jumatatu, ilipofika mwisho wa wiki alikuwa ameishaondoka na ameniacha kwenye deni kubwa sana", alisema Cheeseman alipokuwa akiongea na waandishi wa habari.
Alipotoa taarifa polisi aliambiwa kuwa yeye ni mmojawapo ya wanajeshi wengi walioingizwa mjini na Finley.
Msako mkali unaendelea nchini Marekani kumsaka Finley na taarifa za awali zinasema kwamba jumla ya wanaume 40 wameishajitokeza kuripoti kutapeliwa kwao na Finley.
source nifahamishe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment