Mtoto Huyu Anauzwa

Thursday, May 27, 2010 / Posted by ishak /


Mtoto huyu wa kichina akiwa amefungwa minyororo kwenye mlingoti wa alama za barabarani, anapigwa mnada barabarani na baba yake ambaye ameamua kumuuza ili akatumike kama mtumwa.
Mtoto wa Kichina mwenye umri wa miaka minane akionyesha wazi hofu iliyotanda uso wake, alisimama pembeni ya barabara akiwa amefungwa minyororo na baba yake ambaye alikuwa akijaribu kumuuza mtoto huyo kwa kupiga kelele kama wauza mitumba.

Baba wa mtoto huyo aliyejulikana kwa jina la Yong Tsui aliweka meza ndogo mbele ya mtoto huyo akiandika jina, umri na uwezo wa kufanya kazi wa mtoto wake ambaye aliamua kumuuza kama mtumwa.

Baadhi ya watu waliojitokeza kumnunua mtoto huyo walimuuliza baba yake kiasi cha chakula ambacho mtoto wake anaweza kula, swali hilo liliwakasirisha wasamaria wema ambao walianza kumshushia kipigo baba wa mtoto huyo.

Polisi waliwahi kumuokoa Yong kabla hajauliwa na wakazi wa jimbo la Wuhan, lililopo ukanda wa kati wa China.

Polisi walimchukua mtoto huyo ambaye hivi sasa anapewa matunzo na serikali. Baba wa mtoto huyo aliwaambia polisi kuwa mama wa mtoto wake alifariki miaka mitatu iliyopita na tangu wakati huo amekuwa akipata tabu kumpa matunzo mtoto huyo.

"Hana kazi, nyumba wala pesa, anasema kwamba hakuhitaji pesa kwa kumuuza mtoto wake alikuwa akijaribu kumtafutia maisha bora mtoto wake", alisema mmoja wa maafisa wa polisi.

Yong alisema kwamba alisoma habari ya mtoto wa China, Cheng Jingdan, mwenye umri wa miaka miwili ambaye baba yake alikuwa akimfunga minyororo kwenye mlingoti wakati akiwa kazini kwa kuhofia watu wasimuibe mtoto wake.

Mtoto Cheng alichukuliwa na wasamaria wema na kupewa maisha bora baada ya picha yake akiwa amefungwa kwenye minyororo iliposambazwa kwenye vyombo vya habari.

Yong kwa kujaribu kumuuza mtoto wake alitegemea bahati kama hiyo ingemdondokea na mtoto wake lakini matokeo yake aliokolewa na polisi kutokana na kipigo cha wananchi wenye hasira.


source nifahamishe