Wanaume Waliooana Malawi Waachiwa Huru Baada ya Wafadhili Kupiga Mkwara

Sunday, May 30, 2010 / Posted by ishak /


Wanaume wawili waliooana nchini Malawi ambao walitupwa jela miaka 14 wiki iliyopita kwa kuvunja sheria na kukiuka maadili ya kiafrika wameachiwa huru baada ya Malawi kuelemewa na shinikizo kubwa la mataifa wafadhili.
Baada ya shinikizo kubwa toka nchi za magharibi, serikali ya Malawi imerudi nyuma katika harakati zake za kupambana na tabia ya ushoga na usagaji kwa kuwaachia huru wanaume wawili waliooana ambao walitupwa jela miaka 14 hivi karibuni.

Steven Monjeza, 26, na "Mkewe" Tiwonge Chimbalanga, 20, walitupwa jela miaka 14 wiki iliyopita baada ya kufunga ndoa na kufanya sherehe iliyohudhuriwa na watu 500.

Mataifa ya magharibi yakidai yanatetea haki za binadamu yalipinga kufungwa kwa Monjeza na mwenzake yakisema kuwa Monjeza na mwenzake hawajafanya kosa lolote zaidi ya kupendana kama wanavyopendana watu wengine.

Serikali ya Uingereza ililaani hukumu iliyotolewa dhidi ya Monjeza na mwenzake ikisema kuwa Malawi imekiuka misingi ya haki za binadamu.

Uingereza ambayo ndiyo mfadhili mkubwa wa Malawi, ilisema kuwa inajadili upya msaada wa paundi milioni 80 ambao Malawi hupewa kila mwaka.

Rais wa Malawi, Bingu wa Mutharika, akiongea na waandishi wa habari leo akiwa pamoja na katibu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, aliagiza Monjeza na mkewe waachiwe huru mara moja.

"Hawa vijana wamefanya kosa dhidi ya utamaduni wetu, dini yetu na sheria zetu lakini hata hivyo nikiwa kama mkuu wa nchi nimewapa msamaha na ninaagiza waachiwe huru bila masharti yoyote", alisema rais Bingu wa Mutharika.

Naye katibu wa Umoja wa Mataifa ambaye alikuwepo kwenye mkutano huo na waandishi wa habari uliofanyika ikulu, alimpongeza rais Bingu wa Mutharika kwa uamuzi wake wa kishujaa wa kulinda haki za binadamu na kuwaachia huru mashoga hao wawili.

source nifahamishe