Miaka 10 Jela Kwa Kumuua Dada Yake Aliyepata Mimba Nje ya Ndoa

Tuesday, June 15, 2010 / Posted by ishak /


Mahakama nchini Jordan imemuondolea adhabu ya kifo aliyohukumiwa mwanaume aliyemuua dada yake baada ya kugundua amepata mimba kabla ya kuolewa. Mahakama imeamuru mwanaume huyo atumikie kifungo cha miaka 10 jela.
Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 24 alimuua dada yake mwenye umri wa miaka 26 kwa kumchomachoma na kisu tumboni mara 15 baada ya kugundua dada yake huyo amepata ujauzito kabla ya kuolewa.

Awali mahakama ya mjini Amman, Jordan iliamuru mwanaume huyo ahukumiwe adhabu ya kifo lakini jana mahakama iliamuru mwanaume huyo atumikie kifungo cha miaka 10 jela baada ya familia yake kumuombea msamaha mahakamani.

"Alimuua dada yake baada ya dada yake huyo kumwambia kuwa alifanya mapenzi na mwanaume ambaye alisafiri kwenda kufanya kazi nchini Saudi Arabia", alisema afisa wa mahakama ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Taarifa ya mahakama ilisema kuwa mauaji hayo yalifanyika mwaka jana katika mji wa Karak wakati huo dada yake alikuwa na mimba ya wiki nne.

Kwa mujibu wa sheria za Jordan, mtu anayeua naye huuliwa lakini kwa mauaji yanayoitwa "Kulinda Heshima ya Familia" adhabu ya kifo huondolewa iwapo familia ya mwanamke aliyeuliwa itaiomba mahakama ipunguze adhabu kwa muuaji.

Wanawake 15 hadi 20 huuliwa kila mwaka nchini Jordan kwa staili hiyo hiyo ya kulinda heshima za familia ingawa serikali ya Jordan inafanya jitihada ya kuiondoa tamaduni hiyo potofu.

source nifahamishe