Mwarabu Ampigilia Misumari 24 Hausigeli Wake

Friday, August 27, 2010 / Posted by ishak /


Mfanyakazi wa ndani toka nchini Sri Lanka aliyekuwa akifanya kazi za ndani nchini Saudi Arabia, amerudi kwao akiwa na misumari 24 ndani ya mwili wake ambayo ilipigiliwa na bosi wake kila alipokuwa akilalamika kazi ngumu alizokuwa akipewa.
Picha za X-Ray zilionyesha misumari 24 ikiwa kwenye mwili wa bi L.T. Ariyawathi kwenye sehemu za kichwani, miguuni na mikononi.

Ariyawathi mwenye umri wa miaka 49, aliamua kurudi kwao Sri Lanka baada ya miezi mitano ya kufanya kazi nchini Saudi Arabia, atafanyiwa operesheni kesho kuiondoa misumari toka kwenye mwili wake.

Mfanyakazi huyo wa ndani aliliambia gazeti moja nchini humo kuwa bosi wake raia wa Saudi Arabia alikuwa akimpigilia misumari kama adhabu.

"Walikuwa hawaniruhusu nipumzike, mke wake alikuwa akiipasha moto misumari halafu yeye alikuwa akiipigilia kwenye mwili wangu", alisema Ariyawathi.

Prabath Gajadeera, mkurugenzi wa hospitali ya Kamburupitiya hospital nchini humo ambayo Ariyawathi anapatiwa matibabu alisema: "Picha za X-ray zimeonyesha kuwa misumari 24 na sindano zimo kwenye mwili wake, kuna msumari mmoja kwenye paji lake la uso".

Misumari hiyo yenye urefu wa sentimeta tano ilipigiliwa zaidi kwenye mikono, miguu na viganja vya miguu ya Ariyawathi.

"Hali yake inaendelea vizuri lakini tunampatia antibiotics na dawa za kutuliza maumivu".

Tukio hili limetishia uhusiano wa kisiasa kati ya Sri Lanka na Saudi Arabia.

Kuna raia wa Sri Lanka milioni 1.8 walioajiriwa nje ya nchi. Asilimia 70 kati yao ni wanawake.

Wengi wao hufanya kazi za ndani katika nchi za mashariki ya kati wakati wachache hufanya kazi nchini Singapore na Hong Kong.

source nifahamishe