Semenya Azua Tena Mjadala wa Jinsia Yake

Monday, August 23, 2010 / Posted by ishak /


Mjadala wa jinsia ya mwanariadha wa kike wa Afrika Kusini, Caster Semenya umeibuka tena baada ya Semenya kuwaburuza tena wenzake na kushinda mbio za mita 800 nchini Ujerumani na kuwaacha wanariadha wenzake wakilalamika wanashindana na mwanaume.
Baada ya kudaiwa hakukumbana na nyota wa riadha katika mbio zake za mita 800 nchini Finland, Caster Semenya amewadhihirishia watu kuwa yuko fiti kwa kuwaburuza vigogo wa mbio za wanawake za mita 800 nchini Ujerumani.

Katika mbio hizo zilizofanyika jana mjini Berlin, Semenya aliibuka mshindi kwa kutumia muda wa dakika moja na sekunde 59.90.

Ushindi huo wa Semenya umeibua tena mjadala wa jinsia yake ambapo sasa baadhi ya wanariadha wenzake wameanza kulalamika kuwa wanashindana na mwanaume.

Mwanariadha wa Uingereza Jemma Simpson, ambaye alishika nafasi ya nne kwa kutumia sakika 2 na sekunde 0.57 alilalamika kuruhusiwa kwa Semenya kushiriki mbio za wanawake wakati kukiwa na mjadala wa jinsia yake.

"Wakati mwingine tunajizuia kutoa maoni yetu kuhusiana na jinsia ya Semenya lakini tunasikitishwa sana", alisema Simpson.

Naye mwanariadha wa Kanada, Diane Cummins ambaye alishika nafasi ya nane kwenye mbio hizo hakuficha hasira zake kwa kudai wanashindana na mwanaume.

Diane alisema kuwa wakiwa kama wanariadha wanashindwa kutoa maoni yao binafsi kuhusiana na Semenya kwakuwa wanapotamka yaliyo mioyoni mwao huonekana ni wanamichezo wabaya ambao wanatoa lawama baada ya kushindwa.

Mwanariadha wa Italia, Elisa Cusma Piccione, ambaye alishika nafasi ya tatu alikataa kutoa maelezo ya kauli yake aliyoitoa mwaka jana kuwa Semenya ni mwanaume.

Semenya kwa upande wake alisema kuwa ataanza maandalizi yake kujiandaa na mbio za jumuiya ya madola zitakazofanyika mwezi oktoba.

Semenya aliingia kwenye mbio za jana akiwa amefanya mazoezi kwa mwezi mmoja tu na hakufanya mazoezi ya kuongeza spidi yake.

Inatarajiwa kuwa kwenye mbio za mwezi oktoba atakuwa amerudia fomu yake ya zamani aliyokuwa nayo wakati anaweka rekodi ya dunia kwenye mbio za wanawake za mita 800.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment