Noti mpya bandia sasa zapitia benki

Wednesday, February 16, 2011 / Posted by ishak /

KASHFA ya kukithiri kwa noti mpya bandia inazidi kuongezeka na sasa imebainika kuwa hata baadhi ya benki nchini zinashindwa kuzibaini na hivyo kujikuta zinaziingiza kwenye mzunguko.

Hali hiyo inatokana na Karani wa Fedha wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) Februari 14 kuchukua fedha benki ya CRDB tawi la Lumumba na bila kutambua hatimaye akagundua amepewa noti nyingi za Sh 10,000 zikiwa bandia.

Hata pale mmoja wa wafanyakazi wa TSN aliyepewa noti hizo alipokwenda kuweka baadhi ya noti hizo kwenye moja ya benki bila kujua kuwa ni bandia, karani wa benki hiyo alizipokea na kuzipitisha kwenye mashine na kuridhika kuwa ni halali.

Kitendo hicho kinaonesha kuwa mashine za benki hazizitambui noti hizo na hata wafanyakazi wenyewe wa benki yawezekana hawana utaalamu wa kutosha wa kutofautisha noti bandia na halali hasa za Sh 10,000.

Noti hizo ziligunduliwa na wafanyakazi waliopewa fedha hizo baada ya kuanza kuzitumia na kukataliwa mitaani ambapo jana baadhi yao walijikuta wakiwa na noti hizo.

Meneja wa Fedha wa TSN, Diana Lyatuu, alithibitisha kuchukuliwa fedha hizo kutoka benki ya CRDB tawi la Lumumba kwa kubadilishwa na hundi.

Noti nyingi ambazo zimezagaa ni zinazoishia na namba 366 na 362 ambazo ndizo wafanyakazi wengi wa TSN walikabidhiwa.

Mmoja wa wafanyakazi wa TSN, Nelly Mtema, alikamatwa na Polisi baada ya kuzitumia fedha hizo alizopewa ofisini kwa ajili ya kwenda kulipia bili ya maji katika ofisi za Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO).

Akielezea tukio hilo, Mtema alisema Februari 15 asubuhi alikwenda Dawasco kulipia maji lakini akashangaa kuwekwa chini ya ulinzi kwa maelezo kuwa ana fedha bandia.

“Niliwakatalia kuwa si bandia kwani nililipwa ofisini, lakini nikapelekwa Polisi kituo cha Kimara,” alisema Mtema ambaye baada ya kuzichunguza noti hizo aligundua bandia zikiwa tatu za Sh 10,000.

Aliongeza kuwa baada ya sakata hilo, alilazimika kupiga simu ofisini, kufahamisha kuwa fedha alizopewa ni bandia na amekamatwa na polisi baada ya kuzitumia kulipia huduma ya maji.

“Ofisini walizungumza na polisi juu ya kuwapo tatizo hilo ndipo nikaachiwa,” alisema Mtema.
Mkurugenzi wa Masoko wa CRDB, Tully Mwambapa, alipoulizwa juu ya tatizo hilo, alisema ana uhakika asilimia 100 ya fedha hizo hazikutolewa na benki yake.

“Sisi tuna sheria inayomtaka mteja ahesabu na ahakiki fedha zake kabla ya kuondoka dirishani, itakuwaje keshia aondoke ndipo tupokee malalamiko ya kuwapo fedha bandia?” Alihoji Mwambapa.

Keshia wa TSN alipoulizwa alisema hakuona haja ya kuhakiki fedha hizo kwa vile anaiamini benki hiyo kwani amefanya nayo kazi kwa siku nyingi. Hata hivyo, Mwambapa alisema: “Benki yangu ina sera ya kutoaminiana katika mambo ya fedha.”

Alijitetea kuwa kila dirisha lina kamera inayochukua mwenendo wa matukio ya kuanzia asubuhi hadi jioni yanayofanywa na karani aliyepo kwenye dirisha husika. “Ndiyo maana nasema fedha hizo hazikutoka kwetu,” alisema

Gazeti hili lilitaka kujua ukweli kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutokana na kukithiri kwa noti hizo bandia, lakini simu ya Gavana Benno Ndulu ilikuwa inaita bila majibu.

Baadaye Katibu Muhtasi wa Gavana alisema bosi wake alikuwa kwenye kikao muhimu na akashauri mwandishi kama ni suala hilo la noti bandia uulizwe uongozi wa benki husika kwani utakuwa na majibu ya tatizo hilo.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Mji Mkongwe, Ibrahim Muhamad Sanya (CUF) ametoa hadhari kwa BoT na Hazina juu ya kuzagaa kwa noti mpya bandia na kuvitaka vyombo hivyo kuchukua hatua za haraka kwa kuwa kuna hatari ya uchumi kuathirika.

Sanya alitoa hadhari hiyo na kuwasilisha noti bandia ya Sh 10,000 juzi bungeni wakati wa mjadala wa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, aliyoiwasilisha wakati akifungua Bunge la 10, mwaka jana.

Kwa hadhari hiyo, Spika wa Bunge Anne Makinda, aliitaka Wizara ya Fedha kuwasilisha taarifa juu ya suala hilo bungeni. Akiwasilisha noti hiyo, Sanya alisema iligundulika kuwa bandia baada ya kukaguliwa na kubainika haina picha ya Baba wa Taifa upande wa kushoto.

Alipoulizwa na Spika Makinda alikoipata noti hiyo, alisema alikabidhiwa na mfanyabiashara ndogo mjini Dodoma ambaye alidai kuipata kwa mteja aliyemwuzia bidhaa, hali ambayo ilimtia hasara kwa kuwa kiasi hicho cha fedha ni sawa na mtaji wake.

“Kijana huyo aliponiona alinikabidhi noti hii na kudai kuwa kwa sasa zimezagaa mjini hapa na kunitaka niiwasilishe bungeni ili vyombo husika vichukue hatua, kwa kuwa hali mtaani ni mbaya,” alisema Sanya.

Akipokea taarifa na noti hiyo, Makinda alimshukuru Sanya kwa kutoa taarifa hiyo, na kuitaka serikali ichukue hatua za haraka na kulitolea maelezo suala hilo bungeni.

Tangu kutangazwa kwa noti hizo mpya kumekuwa na malalamiko kadhaa kutoka kwa wananchi wakidai noti hizo hazina ubora na ni rahisi kughushiwa lakini BoT ilijitetea na kudai kuwa zina ubora wa kimataifa na si rahisi kughushiwa.


source habarileo

0 comments:

Post a Comment