Wanawake Wanaovaa Vimini Ndio Wanaotuletea Mabalaa Duniani'

Thursday, April 22, 2010 / Posted by ishak /


Mmoja wa viongozi wa juu wa kidini nchini Iran amesema kuwa wanawake wanaovaa vimini na nguo za kuwadatisha wanaume ndio chanzo cha mabalaa mbali mbali yanayotokea siku hizi kama vile matetemeko ya ardhi na tsunami.
Wanawake wanaovaa nguo zisizo za heshima zinazoyaacha wazi maungo yao wamedaiwa kuwa ndio chanzo cha mabalaa mbali mbali yanayoua maelfu ya watu ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni.

Akiongea katika sala ya ijumaa mjini Tehran nchini Iran wiki iliyopita, mmoja wa viongozi wa juu wa kidini wa Iran, Ayatollah Kazem Sedighi alisema "Wanawake wengi siku hizi hawavai nguo za heshima na matokeo yake wanawachanganya wanaume na kupelekea kuongezeka kwa matendo ya zinaa ambayo ndiyo yanayosababisha matetemeko ya ardhi na mabalaa duniani".

"Majanga yanayotokea duniani yanatokana na madhambi ya watu", aliongeza Ayatollah Sedighi.

"Hatuna njia ya kuepuka kufunikwa na vifusi vya majengo yetu zaidi ya kumrudia mungu na kufuata misingi ya dini yake ya kiislamu", aliendelea kusema Ayatollah Sedighi.

Wanawake nchini Iran hutakiwa kuvaa kwa mujibu ya misingi ya mafundisho ya kiislamu lakini wanawake wengi wamekuwa wakivunja sheria na kuacha wazi sehemu za mbele za nywele zao na pia wengine huvaa nguo zinazobana na kuonyesha maungo yao.

Iran ni miongoni mwa nchi chache duniani zinazosumbuliwa na matetemeko makubwa ya ardhi mara kwa mara.

Mwaka 2003 tetemeko kubwa la ardhi liliukumba mji wa Bam kusini mwa Iran na kuteketeza maisha ya watu 31,000.

Mwanzoni mwa mwezi huu, rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, aliwaonya wakazi milioni tano wa mji mkuu wa Iran, Tehran kuwa waukimbie mji huo kwani tetemeko kubwa la ardhi huenda likatokea wakati wowote.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment