SERIKALI imewataka wanafunzi wa Tanzania wanaosoma nje kufuata maagizo ya serikali yanayowazuia kutembea usiku wanapokuwa ughaibuni na kama ikilazimika kufanya hivyo, basi watembee kwa makundi.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa bungeni jana wakati wa kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mji Mkongwe, Ibrahim Muhammad Sanya (CUF) aliyetaka kujua serikali inachukua hatua gani kwa vifo vya wanafunzi wanaosoma nchi za nje.
Akitoa kauli hiyo baada ya kujibu swali la Msingi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba kuwa pamoja katika safari hizo za usiku kama ikibidi zitaweza kusaidia katika kutoa ushahidi wa nini kilitokea na kusababisha maafa.
Katika swali lake la msingi, Sanya alitaka kujua taarifa ya kifo cha mwanafunzi aliyeuawa huko Bangalore, India hivi karibuni, Imran Mtui na kama serikali ya India imetoa kauli yoyote.
Akijibu swali hilo, alisema India kupitia kwa mkuu wake wa jeshi la polisi wamesema wanaendelea na uchunguzi na pindi utakapokamilika wataieleza serikali ya Tanzania nini kilichojiri.
Hata hivyo, taarifa za awali zilisema kwamba marehemu Mtui alikutwa kandokando ya reli, majira ya saa tatu asubuhi ya Januari 31 mwaka huu akiwa na majeraha makubwa kichwani.
Aidha, taarifa za madaktari wa India zilibaini kwamba, alikufa kutokana na mshituko na kuvuja damu kulikosababishwa na kusagwa kichwa na treni.
Alisema pia ni vigumu kuelewa mambo na kwamba kijana huyo aliyekuwa na kawaida ya kutoka na pikipiki siku hiyo alitoka bila pikipiki.
Aidha, Balozi Iddi alizungumzia mauaji ya Watanzania wanafunzi huko Marekani na kusema, uchunguzi bado unaendelea na ukimalizika pia serikali ya Marekani imesema itatoa taarifa kwa serikali ya Tanzania.
source habarileo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment