aliyeingia uwanjani apata dhamana

Thursday, June 10, 2010 / Posted by ishak /


SHABIKI namba moja nchini Tanzania wa mchezaji wa timu ya Brazil, Ricardo Kaka, ameachiwa huru kwa kupata dhamana ya jeshi la polisi na suala lake litashughulikiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu [TFF
Naggar Ali Kombo alishikiliwa na jeshi la polisi kwa takribani siku tatu kufuatia kitendo cha kuingia uwanjani katika mechi kati ya Brazil na Tanzania iliyofanyika Jumatatu ya wiki hii katika Uwanja mpya wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema, Naggar wamemuachia huru kwa kupata dhamana ya jeshi hilo na dhamana nyingine kutoka kwa baba yake mzazi aliyetambulika kwa jina la Ali Kombo.

Kova alisema baba yake mzazi alijitokeza kumpa dhamana mtoto wake huyo na pia mzazi huyo alimpongeza mwanae huyo kwa kuonesha upenzi wake dhidi ya mchezaji huyo ambaye alikuwa akimpenda kutoka moyoni.

Kova alisema wameamua kumpa dhamana kijana huyo na kuliachia mwenendo mzima wa shauri hilo washughulikie TFF kutokana na kosa lenyewe.

Hivyo Nagaar yuko nje kwa dhamana na TFF limeachiwa kushughulikia mwenendo mzima wa sakata hilo kutokana na kosa lenyewe liko kimichezo zaidi.