Mwanamke Kusalisha Sala ya Ijumaa Uingereza Leo

Friday, June 11, 2010 / Posted by ishak /Kwa mara ya kwanza nchini Uingereza sala ya ijumaa ya waislamu itaongozwa na mwanamke anayepigania usawa wa kijinsia katika dini ya kiislamu.
Mwandishi wa habari wa Kanada, Raheel Raza mwenye umri wa miaka 60 atakuwa mwanamke wa kwanza nchini Uingereza kusalisha sala ya ijumaa.

Raheel ambaye alizaliwa muislamu, amekuwa akipigania usawa wa kijinsia katika dini ya kiislamu.

Raheel amealikwa mjini Oxford nchini Uingereza kusalisha sala ya ijumaa katika jumuiya inayoongozwa na kiongozi wa kituo cha waislamu mjini Oxford, Taj Hargey.

Kwa mujibu wa gazeti la Independent, Taj Hargey anadai kuwa yeye ni Imamu anayepigania sala zenye mchanganyiko wa jinsia na pia anapigania wanawake kuwa maimamu.

Raheel ambaye ni mkazi wa mji wa Toronto nchini Kanada, yeye anapigania usawa wa jinsia katika uislamu na anataka wanawake wapewe nafasi za uimamu na uongozi wa misikiti.

Miaka mitano iliyopita, Raheel alitumiwa vitisho vya kuuliwa baada ya kutoa khutba ya sala ya ijumaa ambayo wanawake na wanaume walichanganyika pamoja. Sala hiyo ilifanyika kwenye mojawapo ya vituo vya taasisi yake.

Raheel atakuwa mwanamke wa pili duniani kusalisha sala ya ijumaa lakini pia atakuwa mwanamke wa kwanza muislamu wa kuzaliwa kusalisha sala ya ijumaa.

Mwaka 2008, mwanamke wa kikristo wa Marekani aliyebadili dini kuwa muislamu na kujiita Amina Wadud aliongoza sala ya ijumaa nchini humo. Hata hivyo sala yake ilihudhuriwa na watu pungufu ya 40 kutokana na maandamano ya kumpinga yaliyofanywa na wanawake wa kiislamu.

Taj Hargey amedai kuwa sala ya leo ya ijumaa itakayoongozwa na mwanamama Raheel itahudhuriwa na watu zaidi ya 100 ambapo kama kawaida wanawake na wanaume watachanganyika na kuasali bega kwa bega.

source nifahamishe