Maalim Seif ataka uchaguzi Zanzibar usogezwe mbele

Friday, January 15, 2010 / Posted by ishak /


KATIBU mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amependekeza uchaguzi mkuu wa Zanzibar mwaka huu usogezwe mbele au Rais Amani Abeid Karume aongezewe muda ili kuweka misingi imara ya kuondoa siasa za chuki visiwani humu.

Hamad alitoa pendekezo hilo jana alipokuwa akiwasilisha mada kwenye kongamano la siku moja la kujadili maridhiano na mustakabali wa Zanzibar lililofanyika kwenye Hoteli ya Bwawani mjini Unguja.

Pendekezo hilo limekuja siku mbili baada ya Rais Amani Abeid Karume kueleza kwenye sherehe za Mapinduzi kuwa hakuna muhula wa tatu kwa urais wa Zanzibar katika hotuba iliyoonekana kama ya kuaga Wazanzibari.

Wakati Karume akionekana kukataa pendekezo hilo ambalo utekelezaji wake unahitaji mabadiliko ya kikatiba, Maalim Seif aliibuka na wazo tofauti katika kongamano hilo lililoandaliwa na chama chake na kushirikisha viongozi mbalimbali wa kisiasa, dini, wasomi na wataalamu wa ndani na nje ya nchi.

"Binafsi nimekuwa nikitafakari sana changamoto hizi na naamini tunapaswa kuzitafakari na kuzijadili kwa lengo la kuona tunazikabili vipi," alisema Seif ambaye aliwahi kuwa waziri kiongozi.

"Ni maoni yangu kuwa tukifanya haraka ya kukimbilia uchaguzi ambao nilishaeleza hapo awali kwamba umekuwa ndiyo chanzo cha kuvurugika kwa umoja wetu, kuna hatari ya kuyapoteza yote niliyoyaeleza.

"Hatuwezi kukwepa uchaguzi maana ndiyo njia ya kidemokrasia ya kuwapata viongozi wetu, lakini tumeshafanya chaguzi saba za vyama vingi Zanzibar, nne kabla ya Mapinduzi na tatu tangu 1992 na zote zimeshindwa kutupa umoja.

"Kwa Zanzibar, katika kipindi hiki, maridhiano ni muhimu zaidi kuliko uchaguzi. Tutapaswa kwenda katika uchaguzi, lakini naamini tutakuwa na uchaguzi mzuri zaidi baada ya kufanikiwa kujenga msingi madhubuti wa maridhiano."

Maalim Seifa alisema baada ya kutafakari kwa kina, ameamua kuungana na wananchi wa Zanzibar zikiwamo taasisi za kidini zinazotaka Rais Karume aongezewe muda au uchaguzi kusogezwa mbele.

Alisema hili litatoa fursa kwa Wazanzibari kuingia katika uchaguzi huo baadaye wakati ukiwa huru na salama zaidi bila matatizo ambayo yamekuwa yakijitokeza miaka ya nyuma.

"Natoa wito wa kuchukuliwa hatua ya kusogeza mbele kidogo uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka huu kwa kipindi cha kati ya mwaka mmoja au miaka miwili ili kutoa nafasi kwa Rais Amani Karume kuchukua hatua zaidi za kukamilisha kazi njema aliyoianza," alisema.

"Naelewa mwenyewe juzi katika hotuba yake ya kilele cha sherehe za Mapinduzi, (Karume) alisema kwamba anakamilisha kipindi chake na katiba ya Zanzibar hairuhusu kipindi cha tatu. Nakubaliana naye na sipendekezi kuondolewa kwa ukomo wa vipindi viwili kwa mtu anayeshikilia madaraka ya urais wa Zanzibar.

"Ila, namwomba sana akubaliane na matakwa ya Wazanzibari walio wengi kama yalivyokwisha onyeshwa kupitia taarifa na kauli mbalimbali kwamba kipindi chake cha pili tukiongeze muda kidogo ili tusiipoteze fursa ya kihistoria ambayo ameianzisha yeye."

Maalim Seif ametoa wito kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa upande wa serikali na upinzani kulitafakari kwa kina jambo hilo na kuwapa Wazanzibari wanachokitaka.

"Nawaomba Wazanzibari tuungane pamoja kumtaka Rais Amani Karume aweke upande dhamira yake ambayo najua anaiamini sana ya kuondoka madarakani mwaka huu na badala yake akubaliane nasi juu ya haja ya kuendelea kuubeba mzigo huu tunaotaka kumtwisha na atuvushe pale ambapo waliomtangulia walishindwa," alisema.

Awali Maalim Seif alianza mada yake kwa kusema: "Mimi na Rais Karume tumekubaliana kuwa hakuna kurudi nyuma katika hatua tuliyoianzisha."

Alisema nia ni kuona kuwa wanaitumia fursa hiyo kuirudisha Zanzibar katika nafasi yake iliyokuwa nayo awali kwa kuwa Wazanzibari wamechoshwa na matatizo wanayoyapata katika kipindi chote kilichopita.

Kwa mujibu wa Maalim Seif ni muhimu kwa Zanzibar sasa sio uchaguzi bali kuondoa siasa za utengano, chuki, ubaguzi, uhasama, ugomvi na visasi na kuweka siasa za umoja, maelewano na mashirikiano.

Mada hiyo ya Maalim Seif iliungwa mkono na watu waliohudhuria kongamano hilo ambao walisema wataendelea kumshawishi Rais Karume kukubali kuendelea na wadhifa wake ili kutoa nafasi ya kurekebishwa baadhi ya kasoro kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Walisema hakuna haja ya kuingia katika uchaguzi wakati inafahamika kila uchaguzi unaofanyika Zanzibar hutawaliwa na vurugu na hatimaye wananchi kupoteza maisha au kujeruhiwa.

Naila Majid Jidawy, mwanasiasa mkongwe ambaye amewahi kushika nyadhifa kadhaa katika vyama tofauti, alisema ipo haja ya kuongezwa muda kwa viongozi wawili Maalim Seif na Rais Karume ili wamalize tofauti zao na mambo waliyokubaliana ili Wazanzibari waingie katika uchaguzi wakiwa na hali ya usalama na amani.

"Maalim mada yake ni kubwa sana katika nchi maana anazungumzia usalama wa Wazanzibari, hazungumzi kama mgombea anataka kugombea kwa maana kwamba huu uchaguzi unaotaka kuja miezi tisa au kumi ijayo hautafanikiwa na hakuna njia ya kufanikiwa na sote tunajua," alisema.

"Kwa maoni yangu binafsi, nataka uchaguzi huu uahirishwe na yeye Maalim na Karume waendelee kwa sababu wao ndio walioyawaza haya na kuzungumza na wakatushushia sisi na wametupa maneno mazito haya ni makubwa sana."

Akichangia mada katika kongamano hilo, mwanafunzi wa mwaka wa nne wa chuo kikuu cha Zanzibar, Zubeir Zubeir alisema iwapo uchaguzi utafanyika hivi sasa, kuna uwezekano wa kuwepo matatizo makubwa.

Aliwataka wanafunzi wenzake na viongozi wote kuunga mkono mazungumzo hayo ili kufanya kazi kwa pamoja kwa kuwa hakuna mtu mwenye hati miliki ya uongozi.

Katibu mkuu wa Chadema Zanzibar, Hamad Yussuf alisema mfumo uliopo ubadilishwe ili atakayekuja aje kukuta mfumo uliopo ambao utawarahisishia wananchi kufaidi matunda yaliyopo kwani kuongezewa muda kwa Rais Karume kunaweza kusababisha matatizo ya kikatiba.

"Rais ana miaka tisa sasa kwa hivyo ni kipndi cha kutosha kama alitaka kuweka mfumo au kuweka chochote. Kwa maoni yangu rais atumie miezi iliyobakia katika baraza la wawakilishi linalokuja ili kurestructure (kujenga upya)mifumo au na kufuta sheria kandamizi badala ya kusema tumuongezee muda," alisema.

Makamu mwenyekiti wa NLD, Mfaume Ali Hassan alisema uchaguzi unaokuja uongezwe muda kwa kuwa huenda watu wakaingia katika mapambano ya lazima.

Wakili maarufu, Awadh Ali Said alisema hakubaliani na maoni ya wengi ya kuongezewa muda Rais Karume akisema ni sawa na kuendeleza udikteta na kuwekeza kwa watu na sio kwa nchi.

source,mmwananchi.co.tz

0 comments:

Post a Comment