Aliyemrushia Bush Viatu Atoka Jela Akiwa Hana Meno Mawili

Wednesday, September 16, 2009 / Posted by ishak /

Mtangazaji wa Iraq ambaye alitupwa jela baada ya kumrushia viatu vyake rais wa zamani wa Marekani George Bush wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa habari nchini humo, ametoka jela jana huku akiwa amepoteza meno mawili kutokana na mkong'oto aliokuwa akipewa jela.
Muntazer al-Zaid mtangazaji wa televisheni ya Iraq ambaye alimfanya rais wa zamani wa Marekani, George Bush apige mbizi mara mbili kuvikwepa viatu vyake namba 10 alivyomrushia wakati akiongea na waandishi wa habari, ametoka jela jana huku akilalamika kuwa aliteswa sana alipokuwa jela.

Zaid amesema kuwa mkong'oto aliokuwa akipewa jela ulipelekea meno yake mawili yang'oke.

Zaid amesema kuwa maafisa wa jela walikuwa wakimtesa kwa kumpa adhabu mbali mbali kama vile kumpiga shoti za umeme, kumchapa kwa kutumia nyaya za umeme na mabomba ya chuma na adhabu zingine mbali mbali za kumtesa.

"Hivi sasa nipo huru lakini nchi yangu haipo huru, mimi sio shujaa lakini nina uwezo wa kuelezea maoni yangu" alisema Zaid na kuongeza "Najihisi kunyanyasika ninapoiona nchi yangu ikitaabika, Baghdad ikichomwa moto na ndugu zangu wakiuliwa" alisema Zaid muda mfupi baada ya kutoka jela.

Zaid alilakiwa na mamia ya ndugu na marafiki zake ambao walimuandalia sherehe kubwa nyumbani kwake na kumchinjia kondoo kusherehekea kurudi kwake nyumbani.

Akiongea kwenye studio za mwajiri wake wa zamani, Zaid alimtaka waziri mkuu wa Iraq, Nouri al-Maliki amuombe radhi kwa adhabu alizopewa na pia alisema atawataja maafisa wa serikali na jeshi waliokuwa wakimtesa jela.

Maisha ya Zaid yamebadilika tangia alipotoka jela kwani bosi wake amemnunulia nyumba mpya kwa ujasiri wake aliouonyesha pamoja na kuifanya televisheni yao iwe maarufu duniani.

Zaid ameahidiwa na wafanyabiashara wa kiarabu magari ya kifahari pamoja na pesa huku wanawake wengi wa Baghdad na ukanda wa Gaza wametangaza kuwania kuolewa naye.

Wakati huo huo taarifa iliyotolewa na familia ya Zaid imesema kuwa Zaid ameondoka jana jioni nchini Iraq kwenda Syria kwa ndege binafsi ambako atakaa kidogo kabla ya kuelekea nchini Ugiriki kwa matibabu ya afya yake.

source.nifahamishe.com

0 comments:

Post a Comment