Chakula Chenye Sumu Kwenye Msiba Zambia

Monday, September 14, 2009 / Posted by ishak /


Zaidi ya waombelezaji 150 katika msiba mmoja nchini Zambia, wamelazwa hospitali baada ya kula chakula kinachohisiwa kuwa na sumu.
Waombelezaji 153 katika msiba mmoja nchini Zambia waliwahishwa hospitali wakiwa hoi taabani baada ya kula chakula kwenye msiba kinachohisiwa kuwa na sumu.

Afisa mmoja wa wizara ya afya wa Zambia alisema kuwa waombelezaji hao walikula ugali wa unga wa mahindi unaoitwa "Nshima" na kunywa pombe ya mahindi inayoitwa "Munkoyo".

Tukio hilo lilitokea kwenye mji wa Luanshya uliopo kilomita 250 toka mji mkuu wa Zambia Lusaka na jumla ya waombelezaji 153 waliwahishwa hospitalini siku ya jumamosi na kulazwa kutokana na sumu iliyokuwemo kwenye vyakula hivyo.

Wagonjwa hao waliwahishwa kwenye hospitali mbili za jirani na wengi wao walilazwa kwenye sakafu za hospitali hizo kutokana na upungufu wa vitanda, taarifa iliyotolewa na shirika la habari la Zambia (ZANIS) ilisema.

"ZANIS ilipotembelea hospitali zote mbili ilikuta wagonjwa wakiwa wamelazwa chini wakiwa wamewekewa dripu na walikuwa wakilalamika kuharisha, kutapika na kuhisi kizunguzungu".

Msemaji wa wizara ya afya, Reuben Mbewe alisema kuwa chakula walichokula inahisiwa kilikuwa na sumu.

"Inabidi tusubiri kukamilika kwa uchunguzi" alisema msemaji huyo wa wizara ya afya.


source.nifahamishe.com