Bi Harusi Mtarajiwa Atoweka Kabla ya Harusi, Maiti yake Yakutwa Ndani ya Ukuta

Monday, September 14, 2009 / Posted by ishak /


Mwanafunzi wa chuo kikuu cha Yale cha nchini Marekani ambaye alikuwa aolewe jana alitoweka siku chache zilizopita kabla ya harusi yake na maiti yake imekutwa jana ikiwa ndani ya ukuta wa chuo hicho.
Mwili wa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Yale University, Annie Le mwenye umri wa miaka 24, ambaye alitoweka siku chache kabla ya harusi yake umepatikana ukiwa umefichwa ndani ya ukuta wa maabara ya chuo chake.

Mwili wake ulikutwa ndani ya ukuta ambao ndani yake kuna uwazi na nyaya za umeme na mabomba ya maji yanapita toka ghorofa moja kwenda nyingine.

Annie Le alikuwa ametoweka kwa zaidi ya siku sita kabla ya polisi kuanza msako mkali wa kumtafuta.

Awali ilidhaniwa kuwa Le alitoweka ili kukwepa kufunga ndoa na mchumba wake.

Lee alionekana siku ya jumanne asubuhi akiingia kwenye jengo la ghorofa tano ambalo ndani yake kulikuwa na maabara ambayo alikuwa akifanya kazi huku akisoma.

Kutoweka kwake kuliwashangaza polisi kwani video kamera za ulinzi zilionyesha jinsi alivyokuwa akiingia kwenye jengo hilo kwenye majira ya saa nne asubuhi lakini kulikuwa hakuna kamera iliyomuonyesha wakati akitoka pamoja na kwamba kulikuwa na jumla ya video kamera za ulinzi 75 zinazolinda eneo hilo.

Zaidi ya polisi 100 na wapelelezi walikuwa wakilifanyia uchunguzi jengo hilo kwa siku kadhaa kuitafuta maiti yake kabla ya jana kufanikiwa kuiona.

Taarifa zilisema kwamba, mwanzoni mwa mwaka huu Le aliandika makala kuhusiana na usalama katika kampasi ya chuo hicho.

Makala yake ilichapishwa kwenye jarida la chuo hicho mwezi februari ikiwa na kichwa cha habari kinachosema "Crime and Safety in New Haven".

Le na mchumba wake Jonathan Widawsky aliyehitimu shahada ya kwanza katika chuo kikuu cha Columbia University walikuwa wafunge ndoa jana jijini New York.

Awali polisi walisema kuwa Widawsky si miongoni mwa watu wanaoshukiwa kufanya mauaji hayo na alikuwa akishirikiana vyema na polisi.

Polisi hawajasema kama kuna mshukiwa yeyote wa mauaji hayo aliyepatikana hadi sasa.

source.nifahamishe.com

0 comments:

Post a Comment