Kikwete ziarani Jordan, Uturuki

Thursday, February 18, 2010 / Posted by ishak /


RAIS Jakaya Kikwete hayuko nchini na ameanza ziara ya mwaliko nchini Uturuki na Jordan kwa mwaliko wa viongozi wa nchi hizo mbili.

Rais Kikwete aliyeondoka nchini jana aliyeongozana na mkewe Salma wakiwemo na wafanyabiashara mbalimbali wa Tanzania.


Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, ilisema jana kuwa Rais Kikwete alipokea na kukubali mwaliko wa kutembelea Uturuki Februari mwaka jana wakati Rais Gul alipotembelea Tanzania kwa ziara ya pili, kwa mwaliko wa Rais Kikwete.

Katika ziara hiyo Rais Kikwete anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, na pia Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan.

Rais Kikwete pia atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Chama cha Wafanyabiashara wa Uturuki, pamoja na mabalozi wa Afrika wanaoziwakilisha nchi zao katika nchi hiyo.

Tanzania na Uturuki zinatarajiwa kutiliana saini mikataba sita ya ushirikiano na pia Rais Kikwete atatunukiwa shahada ya juu (PHD) ya heshima na Chuo Kikuu cha Faith cha Fatih, mjini Istanbul.

Rais Kikwete anatarajiwa kuondoka Uturuki Jumapili, Februari 21, 2010, kwenda Jordan kwa ziara ya siku tatu kwa mwaliko wa Mfalme Abdullah wa Pili.
source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment