Bi Harusi Mwenye Umri wa Miaka 13 Achanwa Sehemu za Siri, Afariki

Sunday, April 11, 2010 / Posted by ishak /


Msichana mwenye umri wa miaka 13 wa nchini Yemen amefariki dunia kutokana na majeraha aliyoyapata kwenye sehemu zake za siri siku nne baada ya wazazi wake kumuozesha kwa mwanaume mwenye umri wa miaka 23.
Tamaduni za wanaume nchini Yemen kuoa wasichana wenye umri mdogo zimezidi kupigwa na vita na makundi ya kutetea haki za binadamu baada ya msichana mwenye umri wa miaka 13 kufariki katika siku ya nne ya ndoa yake.

Msichana huyo kutoka katika mji wa Hajja, kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Yemen, Sanaa, alifariki tarehe mbili mwezi huu ikiwa ni siku ya nne tu baada ya kuozeshwa kwa mwanaume mwenye umri wa miaka 23, alisema Majed al-Madhaji, msemaji wa taasisi ya kutetea haki za wanawake nchini Yemen inayojulikana kama Sisters Arab Forum for Human Rights.

Ripoti ya daktari katika hospitali ya Al-Thawra Hospital ilionyesha kuwa msichana huyo alifariki kutokana na kupoteza damu nyingi sana baada ya kuchanika kwa sehemu zake za siri.
Mume wa msichana huyo amekamatwa na anashikiliwa na polisi.

Taarifa za makundi ya kutetea haki za binadamu zilisema kwamba msichana huyo aliozeshwa baada ya makubaliano kufikiwa baina ya kaka wa marehemu na mume wa marehemu kuwa kila mmoja amuoe dada wa mwenzake ili kupunguza gharama za mahari.

Taarifa zinasema kuwa desturi hiyo ya marafiki kuozeshana madada hufanyika sana nchini Yemen ambako hali ya maisha ni ngumu sana kutokana na kuyumbayumba kwa uchumi. Familia masikini hushindwa kukataa kuwatoa binti zao wakati watu wenye pesa wanapoahidi kutoa mahari kubwa.

Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya mambo ya jamii, zaidi ya robo ya wanawake wa Yemen huolewa wakiwa na umri chini ya miaka 15 kutokana na taratibu za kitamaduni kuamini kuwa mwanamke akiolewa akiwa na umri mdogo hunyooka na kuwa mke bora, atazaa watoto wengi na pia ataepukana na hadaa za wanaume.

source nifahamishe