Mwanaume Mwenye Bahati Mbaya Kuliko Wote Uingereza

Wednesday, April 14, 2010 / Posted by ishak /


Mkulima wa nchini Uingereza Mick Wilary ambaye anadaiwa kuwa ndiye mtu mwenye bahati mbaya kuliko wote nchini Uingereza kutokana na ajali kibao zinazomkumba, amepata ajali kwa mara nyingine tena iliyoivunja miguu yake yote miwili.
Mick Wilary, mwenye umri wa miaka 58 anadaiwa kuwa ndiye mtu ambaye hana tabasamu kutokana na bahati mbaya zinazomkumba na kumfanya akumbwe na ajali mbaya zinazoyatia maisha yake hatarini.

Mick ameishakumbwa na ajali mbaya zaidi ya 30 na ajali hizo zimepelekea kuvunjika kwa mifupa ya viungo vyake 15.

Katika tukio la hivi karibuni, Mick anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini baada ya miguu yake kupondwa na tingatinga.

Katika tukio hilo dereva wa tingatinga akiliendesha tingatinga hilo modeli ya JCB bila ya kuwa mwangalifu, alimgonga Mick na kumbamiza ukutani.

Katika tukio hilo mguu wa kushoto wa Mick ulivunjika na kupinda kuelekea mabegani wakati mguu wake wa kulia ulijeruhiwa na kugeuka ukiangalia nyuma.

Hata hivyo pamoja na ajali hiyo mbaya ya kutisha, madaktari katika hospitali ya Newcastle wamefanikiwa kuiokoa miguu yake na wamesema kuwa ndani ya miezi sita Mick ataweza tena kuitumia miguu yake kutembea.

Ajali ya kuvunjika kwa miguu yake imetokea ikiwa ni miezi michache baada ya kuvunjika kwa enka za miguu yake yote miwili baada ya kuteleza na kuanguka chini alipokanyaga kiazi mviringo.

Miongoni mwa ajali mbaya zilizowahi kumkumba Mick ni kupasuka kwa fuvu la kichwa chake kwenye sakafu alipopigwa mweleka na paka.

Mick pia ameishawahi kuvunjika mbavu, shingo na mikono katika mfululizo wa ajali mbaya zinazoendelea kumkumba ambazo zimeifanya sura yake ikose tabasamu wakati wote.


source nifahamishe