Zanzibar kuendelea kuwa gizani

Sunday, February 28, 2010 / Posted by ishak /

Shirika la umeme Zanzibar (ZECO) limesema haifahamiki huduma ya umeme itarejea lini visiwani humu kwa vile mafundi kutoka ulaya wanaendelea na matengenezo katika kituo cha Fumba Zanzibar na Ras Kilomoni, Tanzania bara.

Hayo yameelezwa na meneja wa shirika hilo, Hassan Ali Mbarouk, alipokuwa akizungumza na Nipashe baada ya kutakiwa kueleza ni lini huduma ya umeme inatarajia kurudi. Zanzibar iliingia gizani tangu Desemba 10 mwaka jana.

Awali Waziri wa Maji, Nishati na ardhi Mansour Yusuf Himid, alitangaza kuwa huduma ya umeme Zanzibar ilitarajia kurejea Februari 20 kufuatia kuwasili kwa mafundi toka Afrika Kusini na Ulaya.

Meneja huyo wa Zeco alisema jana kazi ya matengenezo katika kituo cha Ras Kilomoni Tanzania bara imeshafanyika kwa asilimia 98 tangu walipoanza matengenezo hayo.

“Mafundi bado wanaendelea na matengenezo na ni mapema kueleza lini umeme utarejea na kabla ya kufanya hivyo ni lazima nishauriane na wakubwa wangu,” alisema meneja huyo na kuongeza kuwa kazi ya matengenezo inandelea vizuri.

Meneja huyo alisema kazi iliyobakia katika kituo cha Ras Kilomoni Tanzania bara ni kuunganisha bomba maalum katika kituo hicho kinachopokea umeme toka Kidatu kabla ya kusafirishwa Zanzibar kupitia waya uliotandikwa chini ya bahari.

Aidha, alisema kwamba katika kituo cha Fumba, mafundi toka Ulaya na wazalendo wanaendelea kukamilisha kazi ya kuweka viunganishi katika waya huo na kazi hiyo inaendelea vizuri tangu vifaa vilivyokuwa vikisubiriwa kuwasili Zanzibar.

“Lakini siwezi kusema kazi zilizobakia zitakamilika lini na kurejeshwa kwa umeme ispokuwa kazi inaendelea vizuri na karibu vifaa vyote vilivyokuwa vinasubiriwa vimewasili Zanzibar,” alisema meneja huyo.

Hata hivyo habari zilizopatikana toka katika vyanzo vya kuaminika ndani ya shirika hilo, zinaeleza kuwa huenda huduma ya umeme Zanzibar ikarejea Machi 3, mwaka huu.

Meneja huyo aliwataka wananchi waendelee kuwa na subira na baada ya kukamilika kwa matengenezo shirika litawatangazia siku ya kurejea huduma hiyo.

Waya unaopokea umeme toka Tanzania Bara uliozikwa chini ya bahari tayari umemaliza muda wake wa matumizi wa miaka 30 na hiyo ni mara ya 3 kulipuka na kusababisha wananchi kukosa huduma ya umeme.

Waya huo unauwezo wa kupokea megawati 45 za umeme wakati matumizi ya umeme yamefikia megawati 43.7.

Tangu kukosekana kwa huduma ya umeme shirika hilo limekuwa likipata hasara ya sh bilioni 2.2 kila mwezi na viwanda vingi vimelazimika kufungwa kutokana na tatizo la umeme pamoja na baadhi ya hoteli za kitalii Zanzibar.

Awali SMZ ilitangaza huduma ya umeme Zanzibar ingetarajia kurejea leo lakini hali imekuwa tofauti.

Kukosekana kwa huduma ya umeme kumesababisha sherehe za kuzaliwa mtume Mohammed kushindwa kufanyika juzi usiku katika viwanja vya Mnazi Mmoja kama ilivyozoeleka na badala yake zilifanyika kuanzia saa 10 jioni katika msikiti wa mwembe shauri na kuongozwa na Rais wa Zanzibar alhaji Amani Abeid Karume.

Mei Mwaka 2008 wananchi wa Zanzibar walilazimika kukaa bila umeme kwa muda wa mwezi mmoja baada ya waya unaopokea umeme kulipuka katika kituo cha Fumba na serikali kulazimika kuagiza wataalamu kutoka Afrika Kusini na Norway.

source ippmedia