Wezi Wapora Duka na Kumsahau Mtoto Wao

Wednesday, March 03, 2010 / Posted by ishak /


Polisi nchini Marekani wanawatafuta wezi waliovamia duka moja la madini na vito vya thamani na kuiba kabla ya kukimbia na kumuacha mtoto wao.
Polisi wa Philadelphia nchini Marekani wanawatafuta wezi wawili walioiba vito vya thamani kwenye duka moja mjini humo kabla ya kukimbia na kumuacha mtoto wa kiume wa miaka minne.

Polisi walisema kuwa mwanaume na mwanamke waliingia kwenye duka la Platinum & Ice Jewelry wakiwa na mtoto na kuomba waonyeshe baadhi ya pete.

Ghafla wezi hao walichukua trei lililokuwa limejaa pete za dhahabu zenye thamani ya jumla ya dola laki moja na kukimbia nalo.

Wezi hao walimburuza mtoto huyo mita chache kabla ya kumtelekeza baada ya mmoja wa wafanyakazi wa duka hilo kuwakimbiza.

Polisi wanaendelea kuwatafuta wezi hao ambao walifanikiwa kutoweka eneo hilo na trei hilo la pete za dhahabu.

Mtoto wao amechukuliwa na kuhifadhiwa kwenye nyumba ya ustawi wa jamii.

source nifahamishe