Rubani Mwenye Vyeti Feki Aendesha Ndege Kwa Miaka 13

Friday, March 05, 2010 / Posted by ishak /


Maafisa wa Uholanzi wamemkamata rubani feki raia wa Sweden ambaye kwa kutumia vyeti feki vya urubani amekuwa akiendesha ndege za abiria kwa miaka 13 bila kugundulika.
Rubani huyo mwenye umri wa miaka 41 alitiwa mbaroni kwenye uwanja wa ndege wa Schiphol mjini Amsterdam akijiandaa kuirusha ndege ya abiria 101 toka Uholanzi kuelekea Uturuki.

Rubani huyo mwenye makazi yake mjini Milan nchini Italia kwa miaka 13 alitumia vyeti feki na kufanikiwa kuendesha ndege za abiria za mashirika ya ndege ya Uingereza, Italia na Ubelgiji.

Kufuatia taarifa waliyotonywa na maafisa wa Sweden, maafisa wa Uholanzi walimnyanyua rubani huyo toka kwenye kiti cha rubani wakati akijiandaa kuanza safari ya kuelekea Uturuki akiwa na abiria 101 kwenye ndege aina ya Boeing 737.

Taarifa zilisema kuwa rubani huyo aliwahi kuwa na leseni ya kuendesha ndege ndogo ambayo pia ilikuwa imeisha muda wake na alikuwa haruhusiwi kuendesha ndege kubwa.

Wakati anakamatwa rubani huyo ambaye jina lake liliwekwa kapuni alikuwa akiendesha ndege ya shirika la Uturuki la Corendon Airlines.

Rubani huyo amewekwa mahabusu mjini Amsterdam akisubiria kufikishwa mahakamani kwa makosa ya kufoji vyeti na kuendesha ndege bila leseni.

source nifahamishe