Kukopa Harusi Kulipa Matanga

Thursday, March 04, 2010 / Posted by ishak /


Mwanaume mmoja wa nchini China ambaye alikuwa akisumbuliwa na madeni mengi sana yaliyotokana na tabia yake ya kupenda kucheza kamari amejiua mwenyewe kwa kujilipua kwa bomu ndani ya basi lililokuwa limejaa abiria.
Kwa mujibu wa shirika la habari la China, Xinhua mwanaume huyo alijilipua mwenyewe ili kuepukana na madeni mengi anayodaiwa ambayo alikuwa hana uwezo wa kuyalipa.

Yang Yongshou, 42, ambaye zamani alikuwa muuza madawa ya kulevya kabla ya kuangukia kwenye uchezaji wa kamari, alijilipua kwa bomu aliloliweka chini ya kiti chake kwenye basi la abiria lililokuwa likifanya safari zake katika jimbo la Yunnan lililopo karibu na mpaka wa Vietnam.

"Yang alikuwa hana uwezo wa kulipa yuan 100,000 (Tsh. Milioni 19.8) ambazo alikuwa akidaiwa kwenye kamari", ilisema taarifa ya polisi.

Yang alifariki hapo hapo kutokana na bomu hilo huku abiria wengine 11 wa basi hilo wakipata majeraha mbalimbali.

Tabia ya watu kujilipua kwa mabomu wanapozidiwa na matatizo imekuwa ikiongezeka kwa kasi sana nchini China ambapo sababu kubwa inasemwa kuwa ni uhaba wa kazi na kuongezeka kwa tofauti ya kipato kati ya watu masikini na matajiri.

source nifahamishe