Madaktari Watupiana Makonde Chumba cha Uzazi

Tuesday, August 31, 2010 / Posted by ishak /


Mama mmoja wa nchini Italia pamoja na mtoto wake mchanga wanapigania maisha yao ambayo yameingia hatarini kufuatia ugomvi mkubwa uliozuka kwenye wadi ya uzazi baina ya madaktari wawili ambao walitakiwa kumzalisha mwanamke huyo.
Ugomvi mkubwa ulioisha kwa madaktari kujeruhiana na kutoana ngeu umepelekea maisha ya mama mmoja wa nchini Italia na mtoto wake mchanga yaingie hatarini.

Laura Salpietro, 30, alipoteza damu nyingi sana wakati wa uzazi na mtoto wake mchanga wa kiume aliyepewa jina la Antonio, alikumbwa na shambulio la moyo mara mbili kwenye wadi ya uzazi katika hospitali iliyopo Messina, Sicily.

Ugomvi mkubwa wa madaktari huo ulianza wakati bi Laura alipowasili hospitali akiwa amezidiwa na uchungu na hali yake ikiwa mbaya sana, madaktari katika hospitali hiyo walianza kubishana watumie njia ya asili au njia ya operesheni kumzalisha bi Laura.

Mabishano hayo kati ya dokta Vincenzo Benedetto na daktari wa wadi ya uzazi Antonio De Vivo yaligeuka kuwa ugomvi na madaktari hao walianza kurushiana makonde ya nguvu ndani ya wadi hiyo.

Mume wa bi Laura, Matteo Molonia alisema kuwa aliwasihi madaktari waache kupigana na wamsaidie mkewe ambaye hali yake ilizidi kuwa mbaya lakini madaktari hao hawakumsikiliza.

"Nipo kwenye hatihati ya kupoteza familia yangu kwasababu madaktari wameamua kupigana ndani ya wadi ya uzazi", alisema Molonia.

Hatimaye bi Laura alijifungua kwa njia ya operesheni lakini kutokana na kucheleweshwa kujifungua, maisha yake na ya mtoto wake yameingia hatarini.

Madaktari wote wawili wamesimamishwa kazi kwa muda wakati uchunguzi wa suala hilo ukiendelea.

Mume wa bi Laura amesema kuwa ana mpango wa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya madaktari hao.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment