Urefu Wasababisha Aache Shule ya Msingi

Friday, September 03, 2010 / Posted by ishak /


Msichana mwenye umri wa miaka 14 wa nchini Brazili ambaye ana urefu wa sentimita 206 amelazimika kuacha shule kwasababu amechoka kujipinda kwenye mabasi wakati wa kwenda shule, ameamua kuingia kwenye fasheni za mavazi.
Elisany Silva pamoja na kuwa na umri mdogo, ana urefu wa sentimita 206 na bado anaendelea kukua.

Elisany ameacha shule ya msingi na sasa anajiandaa kushiriki kwenye shoo yake ya kwanza ya fasheni za mavazi.

Kutokana na urefu wake Elisany anasema kuwa amechoka kujipinda kwenye mabasi wakati wa kwenda shule na pia anashindwa kucheza na watoto wenzake ambao amewazidi urefu zaidi ya nusu mita.

Urefu wake unasababishwa na maradhi ambayo hayajajulikana hata hivyo wazazi wake ambao ni masikini na hawana pesa za kulipia gharama za uchunguzi wa maradhi yake au kumpatia tiba, hawana mpango wa kujua ugonjwa alio nao.

"Nashindwa kufanya shughuli kama watoto wenzangu, nataka nicheze na marafiki zangu lakini siwezi", alisema Elisany.

"Napata shida ninapokuwa ndani ya nyumba yetu, nalazimika kujipinda ninapopita milangoni na mara nyingi sana najigonga kwenye paa la nyumba", aliendelea kusema Elisany.

Pamoja na matatizo ya familia yake, Elisany anatarajiwa kuwa nyota wa dunia wa baadae kwenye fasheni za mavazi kwani anarajiwa kuwa mwanamitindo mrefu kuliko wote duniani akivunja rekodi inayoshikiliwa na mrembo wa California, Marekani, Amazon Eve ambaye ana urefu wa sentimeta 205.

Elisany anatarajiwa kushiriki kwenye shoo yake ya kwanza ya mavazi katika mji wa Belem nchini Brazili ambapo atavaa shela za harusi.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment