Ajinyonga Baada ya Kunyimwa Mkopo

Friday, September 03, 2010 / Posted by ishak /


Mwanaume mmoja wa nchini Uturuki amejinyonga kwenye mlango wa kuingia kwenye sehemu aliyokuwa akifanya kazi baada ya kunyimwa mkopo na kampuni yake.
Mwanaume huyo aliyetajwa kwa jina la Isa Uguten mwenye umri wa miaka 45, alijinyonga kwenye mlango wa kuingia kwenye uwanja wa klabu ya farasi ya mjini Adana ambako alikuwa akifanya kazi kama mtunza bustani.

Taarifa iliyotolewa ilisema kuwa kutokana na matatizo ya kifedha yaliyokuwa yakimkabili, Isa aliamua kuomba mkopo wa fedha toka kwa kampuni yake ambayo amekuwa akiifanyia kazi kwa miaka 15 sasa.

Hata hivyo kampuni yake ilikataa kumkopesha.

Baada ya kuambiwa hivyo, juzi usiku, Isa aliamua kujinyonga kwenye mlango wa kuingia kwenye viwanja vya klabu hiyo.

Mwili wake uligundulika jana asubuhi ukiwa unaning'ia kwenye mlango.

Polisi waliushusha chini mwili wake na aliposachiwa ilikutwa barua kwenye mfuko wake wa suruali akielezea sababu ya kujinyonga huku akiushushia lawama uongozi wa klabu hiyo.

Mwili wa Isa ulikabidhiwa kwa ndugu zake baada ya kukamilika kwa taratibu za uchunguzi wa maiti.

source nifahamishe