BREAKING NEWS - Mwanamke Ampiga Mwereka Papa Benedict Wakati wa Misa ya Krismasi

Friday, December 25, 2009 / Posted by ishak /


Mwanamke mmoja wa nchini Italia anashikiliwa na polisi baada ya kuruka vizuizi vya ulinzi na kumpiga mwereka Papa Benedict XVI wakati akielekea kufungua misa ya krismasi katika kanisa la St. Peter mjini Vatican.
Mwanamke aliyefanikiwa kuruka vizuizi vya ulinzi, alimpiga mwereka Papa Benedict XVI aliyekuwa akielekea mbele ya kanisa kuanzisha misa ya krismasi katika kanisa la St Peter mjini Vatican.

Katika tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia leo ijumaa, Mchungaji Ciro Benedettini aliyekuwa karibu na Papa alisema kuwa Papa aliamka kutoka chini mwenyewe baada ya kuangushwa na mwanamke huyo.

Papa mwenye umri wa miaka 82 hakupata jeraha lolote katika tukio hilo lakini alionekana kutetereka wakati walinzi na wasaidizi wake walipokuwa wakimuongoza kuelekea kwenye altare kuu kuiongoza misa ya krismasi.

Mchungaji Benedettini alisema kuwa mwanamke aliyemwangusha chini Papa alionekana kuwa na matatizo ya akili na alikamatwa na polisi wa Vatican.

Pia mwanamke huyo alimsukuma na kumwangusha chini kardinali Roger Etchegaray, ambaye alipelekwa hospitali kwa uchunguzi zaidi wa afya yake.

Baada ya tukio hilo Papa aliiongoza misa ya krismasi kama kawaida na hakugusia hata kidogo tukio la kuangushwa chini na mwanamke huyo.

Aliianzisha misa ya Krismasi kama ilivyo desturi kwa maneno ya kilatino ya kuwatakia watu amani kwa kusema "Pax vobis" ("Amani iwe juu yenu") na waumini walijibu "Et cum spiritu tuo" ("Iwe juu yako pia").

Hii ni mara ya pili kwa mwanamke kuruka viunzi vya ulinzi na kujaribu kumdondosha Papa. Wakati wa misa ya mwaka jana, mwanamke mmoja aliviruka vizuizi vya ulinzi na kumfikia Papa lakini kabla hajafanya chochote walinzi walimwahi na kumweka chini ya ulinzi.

Haijajulikana mara moja kama mwanamke aliyemdondosha Papa safari hii ndio yule yule wa mwaka jana au la.


source.nifahamishe