Mfanyabiashara wa Kihindi Akamatwa na Kilo 8 za Almasi

Wednesday, December 23, 2009 / Posted by ishak /


Mfanyabiashara mmoja toka India amekamatwa nchini Jamhuri ya Kongo akiwa na begi lililojaa zaidi ya kilo nane za madini ya almasi yasiyosafishwa akijaribu kuyasafirisha madini hayo kinyemela toka nchini humo.
Mfanyabiashara huyo aliyetajwa kwa jina la Ajudiya Pravin Kumar amehukumiwa kwenda jela miezi sita pamoja na kulipa faini ya dola laki moja za Kimarekani.

Kumar ambaye ni mfanyabiashara wa madini ya almasi alikuwa akiendesha biashara zake nchini humo kwa zaidi ya miaka sita.

Kumar alikuwa akitafutwa na mahakama kuu ya Gombe, Kinshansa akituhumiwa kusafirisha kiholela, kumiliki isivyo halali madini ya almasi na kujaribu kuwahonga maafisa wa Jamhuri ya Kongo.

Awali mwendesha mashtaka wa serikali alitaka Kumar ahukumiwe kwenda jela miaka 17 pamoja kulipa faini ya dola milioni 500 kwa hasara ambayo ameisababishia serikali ya Kongo.

Lakini hakimu wa kesi hiyo aliamua Kumar atumikie kifungo cha miezi sita jela pamoja na kulipa faini ya dola 100,000 huku madini hayo ya almasi yakitaifishwa kwa serikali.

Madini hayo yalipofanyiwa utafiti na wataalamu wa madini wa Jamhuri ya Kongo, yaligundulika kuwa na uzito wa karati 42,000 na yakiwa na thamani ya dola 500,000.

Wakili wa serikali alipinga hukumu iliyotolewa akisema haitoi funzo kwa wafanyabiashara wengine wanaouza almasi kimagendo na aliongeza kuwa anasubiria waziri wa sheria atoe malalamiko yake kwa hukumu hiyo.

Kumar alikamatwa tarehe 10 mwezi huu kwenye uwanja wa ndege wa Kinshansa akijaribu kuyasafirisha madini hayo aliyoyaficha kwenye begi lake akiyapeleka India.

Wakati wa taratibu za ulinzi uwanjani hapo, polisi mwanamke wa uwanja wa ndege alikuta mfuko wa Rambo ndani ya begi la Kumar ukiwa na madini ya almasi ambayo yalikuwa hayana hati husika za kuyasafirisha nje ya nchi hiyo.

Katika utetezi wake Kumar alijitetea kuwa alikuwa hana nia ya kusafirisha madini ya almasi akiendelea kusema kuwa alikuwa hajui kuwa amenunua almasi yeye alijua amenunua vito kwa ajili ya kutengenezea shanga na vidani vya wanawake.

source.nifahamishe.com

0 comments:

Post a Comment