Yanga Yaiua Simba Yatinga Fainali Tusker Cup

Friday, December 25, 2009 / Posted by ishak /


YANGA imefanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Tusker baada ya kuifunga Simba mabao 2-1 kufuatia mchezo wa nusu fainali uliochezwa leo jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga ndio waliokianza kipindi cha kwanza kwa kasi na kusukuma mashambulizi langoni mwa Simba katika dakika ya kwanza tu ya mchezo nusura waandike bao baada ya mabeki wa Simba na kipa wao Juma Kaseja kujichanganya lakini Jerry Tegete akawa mziko kuuwahi mpira uliokuwa unazubaa.

Wanajangwani waliendelea kushambulia mfululizo lakini katika dakika ya tano, Simba walizinduka na Mussa Hassa Mgosi alipiga shuti kali lililokua linajaa wavuni lakini kipa Mghana wa Yanga, Yaw Berko aliliona na kupangua na kuwa kona tasa.

Dakika moja baadaye, Mrisho Ngassa aliambaa na mpira tokea katikati ya uwanja huku mabeki wa Simba wakishindwa kumthibiti na alifanikiwa kupiga krosi ‘ndizi’ ambayo hata hivyo beki Kelvin Yondani aliiwahi na kuitoa nje na kusababisha kona ambayo hata hivyo haikuzaa bao.

Kiungo mpya wa Simba, Jerry Santo nusura aipatie timu yake bao katika baada ya kuachia shuti kali pembeni mwa uwanja lakini mara nyingine, Berko alikuwa makini na kupangua mpira huo uliozaa kona.

Kwa ujumla katika kipindi cha kwanza, Yanga ndio waliotawala kipindi cha kwanza na kufanya mashambulizo mengi zaidi wakifanikiwa kutengeneza nafasi saba za kkufunga huku watani wao Simba wakitengeneza nafasi tatu tu.

Katika kipindi hicho Yanga ilipata kona tatu na watani wao Simba wakapata tatu lakini hakuna iliyozaa bao. Huku mwamuzi kutoka Uganda akiwazawadia kadi za njano wachezaji Amir Maftah, Ngassa (Yanga), Yondani na Emmauel Okwi (Simba).

Yanga ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 67 kupitia kwa Jerry Tegete baada ya pasi nzuri iliyopigwa na Abdi Kassim kuuvuka ukuta wa Simba uliokuwa ukijichanganya tangu mwanzo wa mechi.

Baada ya bao hilo Simba walionekana kuchanaganyikiwa na kuwapa nafasi Yanga kushambulia zaidi hata hivyo hawakuwa makini kumalizia.

Dakika ya 78 Okwi aliangusha ndani ya eneo ya eneo la hatari na Cannavaro na mwamuzi kuamuru penalti ipigwe na Hilary Echesa akafunga kwa ufundi huku kipa Obren Cuckovic aliyeingia katika kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Berko aliyeumia akishindwa kuzuia.

Mabao hayo yalidumu hadi dakika 90 na mwamuzi Dennis Batte wa Uganda kuamua kuongeza dakika ambapo katika dakika ya 120, Shamte Ally aliipatia Yanga bao la pili na laushindi baada ya kuitumia vema pasi ya Mrisho Ngassa.

Kwa matokeo hayo, Yanga itacheza na Sofapaka katika mchezo wa fainali keshokutwa Jumapili.

source.nifahamishe

0 comments:

Post a Comment