Mtanzania Auliwa Kwa Kuchomwa Kisu Uingereza

Wednesday, December 23, 2009 / Posted by ishak /


Kijana wa Kitanzania mwenye umri wa miaka 18 aliyekuwa akiishi na kusoma nchini Uingereza ameuliwa kwa kuchomwa kisu na kijana wa Kiingereza mwenye umri wa miaka 15 aliyekasirishwa na maoni mabaya aliyoyatoa kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Kijana wa Kitanzania Salum Kombo aliyekuwa akiishi na kusoma nchini Uingereza ameuliwa na rafiki yake wa karibu kijana wa Kiingereza mwenye umri wa miaka 15 aliyekasirishwa na maoni ambayo Salum aliyaandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Salum aliuliwa kwa kuchomwa na kisu shingoni na begani kwenye uwanja wa basketball uliopo karibu na nyumbani kwao.

Taarifa zilizopatikana zilisema kwamba rafiki huyo wa Salum aliandika maoni kwenye ukurasa wake wa Facebook akionyesha hasira zake kwa kutoalikwa katika party iliyoandaliwa na rafiki zake.

Salum alijibu maoni hayo kwa kuandika maoni ya kumkashifu rafiki yake huyo ambaye kutokana na kukasirishwa kwake alitishia kumuua lakini hakuna mtu aliyetilia maanani vitisho hivyo.

Salum ambaye alikuwa akisomea Sanaa kwenye chuo cha Tower Hamlets College jijini London alikutana na rafiki yake huyo kwenye uwanja wa basketball uliopo karibu na nyumbani kwao ambapo bila kutarajia rafiki yake huyo alimshambulia kwa kumchoma na kisu mabegani na shingoni.

Katika tukio lililotokea siku ya jumapili jioni mbele ya marafiki zake, Salum alijaribu kujikongoja kuelekea kwao huku damu kibao zikimtiririka lakini hakufika mbali na alifariki dakika chache baadae wakati akipewa huduma ya kwanza kwenye eneo la tukio hilo.

Muuaji wake amekamatwa na alipandishwa kizimbani jana jijini London.

Salum aliwasili Uingereza miaka saba iliyopita na alikuwa akiishi na shangazi yake jijini London.

Salum amekuwa kijana wa 13 ndani ya mwaka huu kuuliwa kutokana na mashambulizi ya visu jijini London.

source.nifahamishe.com
om