Faza Krismasi Safari Hii Hakutoa Zawadi, Apora Pesa

Friday, December 25, 2009 / Posted by ishak /


Faza Krismasi huyu wa nchini Marekani hakuwa kama wenzake, hakuja kwa nia ya kutoa zawadi kama kawaida, yeye alivamia benki na kupora pesa.
Mwanaume mmoja wa nchini Marekani akiwa amevalia mavazi ya Faza Krismasi (Santa) aliiteka benki katika mji wa Nashville, Tennessee na kupora pesa na kisha kutoroka.

Faza Krismasi huyu ambaye tofauti na wenzake ambao hubeba zawadi, yeye alibeba bunduki na kuwatishia wahudumu wa benki ya SunTrust Bank wasalimishe pesa zote walizo nazo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na polisi, faza krimasi huyu wa bandia jana asubuhi aliingia kwenye benki hiyo akiwa na kiroba chekundu ambacho alikiweka juu ya meza ya mhudumu wa benki na kisha kutoa bunduki yake akiwaamuru watu wote waliokuwepo kwenye benki hiyo walale chini.

Baada ya kukijaza kiroba chake pesa, faza krismasi huyo alitoka taratibu na kupanda gari la rangi ya kijivu lililokuwa likimsubiria nje ya benki hiyo.

Wakati akiondoka zake, faza krimasi huyo aliwaambia watu waliokuwepo kwenye benki hiyo kuwa "Faza Krismasi anahitaji pesa za kuwalipa wasaidizi wake".

Kiasi cha pesa kilichoibwa toka katika benki hiyo hakijajulikana na polisi wameanzisha msako wa kumtafuta faza krimasi huyo feki.

source.nifahamishe.com