Drogba Aifunga, Aipongeza Taifa Stars

Wednesday, January 06, 2010 / Posted by ishak /


HUKU akiwa mfungaji wa bao pekee na la ushindi la Ivory Coast, mshambuliaji wa Chelsea Didier Drogba amesema Taifa Stars inastahili pongezi kutokana na soka ililocheza katika mchezo wao wa kirafiki uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa,Dar es Salaam
Drogba alisema, awali walitahadharishwa kuhusu uwezo wa Stars lakini hawakuwa na uthibitisho wa kile walichoambiwa; “Tuliambiwa timu ni kali, lakini hatukupata nafasi ya kuangalia kumbukumbu yoyote, na ndicho kilichotokea Uwanjani.”

Katika mchezo huo, Drogba aliweza kuifungia timu yake bao pekee la ushindi kwenye dakika ya 39 kwa kichwa akiunganisha krosi ya chinichini kutoka upande wa kulia wa Uwanja.

Naye Kocha wa Ivory Coast, Vahid Halilhodžic alisema kiufundi Stars ilicheza vizuri na ni moja kati ya timu zinazoweza kuja kufanya vizuri katika siku za usoni katika soka la Afrika.

“Timu ni nzuri, ina speed nzuri, wachezaji wengi wanajua wanachokifanya Uwanjani, pia wameweza kutumia vema kucheza nyumbani,” alisema Halilhodžic.

Naye Kocha wa Taifa Stars, Marcio Maximo alisema; “Tumecheza katika kiwango cha kuridhisha, tumeonesha kwamba tunaweza kucheza na timu nyingine zaidi ya Ivory Coast.”

Ivory Coast ipo jijini Dar es Salaam kwa kambi ya muda ya mazoezi kabla ya kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika itakayofanyika kuanzia Januari 10 m waka huu.

Timu hiyo keshokutwa Alhamisi itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Rwanda ‘Amavubi’ kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

source nifahamishe.com

0 comments:

Post a Comment