Rais wa Afrika Kusini Aoa Mke wa Tatu, Wanne Anasubiria

Wednesday, January 06, 2010 / Posted by ishak /


Rais wa Afrika Kusini ameoa mke wa tatu katika sherehe za kitamaduni zilizofanyika chini ya ulinzi mkali katika mji wa KwaZulu-Natal huku taarifa zaidi zikisema kuwa ataongeza mke wa nne hivi karibuni kwa kumuoa mchumba wake mpya.
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amefunga ndoa kwa mara ya tano katika sherehe kubwa za harusi zilizohudhuriwa na wafanyabiashara, wanasiasa na watu wengi maarufu.

Rais Zuma alikuwa afunge ndoa na mchumba wake Thobeka Mabhija mwenye umri wa miaka 36 mwaka jana lakini sherehe za harusi ziliahirishwa kutokana na shuguli za kisiasa za rais Zuma.

Rais Zuma awali alioa mara nne lakini mke wake mmoja alifariki wakati mke wake mwingine aliachana naye.

Wake wa sasa wa rais Zuma ni Sizakele Khumalo, aliyemuoa mwaka 1973, na Nompumelelo MaNtuli-Zuma, aliyemuoa mwaka 2007.

Wake hao wawili wa rais Zuma walihudhuria sherehe hiyo iliyofanyika Nkandia,KwaZulu-Natal ambapo waandishi wa habari walipigwa stop kuikaribia nyumba ya rais Zuma ambako sherehe hiyo ya kitamaduni ilikuwa ikifanyika.

Ndoa za rais Zuma zimewaganya watu wengi huku vijana wa kisasa wakisema kuwa hazina nafasi katika dunia hii ya kisasa.

Kwa mujibu wa tamaduni za Zulu, wake wawili wa Zuma wanalazimika kumkubali mke mpya atakayejiunga nao na pia wanatakiwa kuhudhuria sherehe za harusi yake.

Wakati huo huo taarifa zaidi zinasema kuwa rais Zuma mwenye umri wa miaka 67 anatarajia kuongeza mke wa nne katika siku zijazo.

Wiki iliyopita mchumba wake mpya Gloria Bongi Ngema alipeleka zawadi za kitamaduni za harusi kwenye familia ya rais Zuma.

Rais Zuma ana jumla ya watoto 18.


source.nifahmishe

0 comments:

Post a Comment