Kakobe na Waumini Wake Wakesha Kulinda Tanesco Wasipitishe Umeme

Wednesday, January 06, 2010 / Posted by ishak /


Askofu Mkuu wa kanisa la Full Gospel Bible fellowship lililopo Mwenge jijini Dar es salaam na wauminini wake wameweka kambi nje ya kanisa hilo ili kuishinikiza Tanesco wasipitishe umeme mkubwa karibu na kanisa lao.
Kakobe na waumini wa kanisa lake wameweka kambi kwa muda usiojulikana wakiwa wamevalia sare ya tisheti zenye maneno ya kuibeza Tanesco na Serikali yenye ujumbe unaosomeka kwa mbele "Tanesco mwogopeni Mungu" na nyuma "Baada ya richmond mmegeukia kanisa!!".

Askofu mkuu wa kanisa hilo Zacharia Kakobe amesema kuwa endapo umeme huo utapitishwa pale jamii itarajie mpambano baina yao na Tanesco.

Kakobe aliwataka Tanesco kwenda kujifunza kwake masuala ya umeme kwani amesoma kuliko wao na watarajie kupata upinzani mkubwa kutoka kwa waumini hao wenye uelewa mkubwa wa athari ya ememe huo.

Alisema kinachofanya waumini hao kukesha hapo kwa muda wote ni kutokana na kutojua ni muda gani nyaya hizo zitapitishwa eneo hilo, hivyo wameona bora waendelee kuwepo kwa muda wote ili kuhakikisha hazipitishwi.

"Huu ni ufisadi unaofanyika hapa,na tutakuwa hapa mpaka kieleweke hata kama ni mwaka mzima kwani huu umeme chuo kikuu waliukataa kutokana na madhara yake hivyo sisi hatuutaki pia na tutapambana" alisema Askofu Kakobe.

Aidha alisema kuwa ujumbe katika tisheti hizo utakuwa unabadilika kulingana na matukio yatakayokuwepo kwani hawatojali gharama kwani uhuru ni gharama kubwa kuliko fedha zinazotumika kutengeneza tisheti hizo.

Aidha Askofu Kakobe aliilaumu Serikali kwa kusema kuwa imekuwa na upendeleo kwa misikiti katika operesheni zake tofauti na inavyofanyika katika makanisa ya kiroho.

"Serikali inapendelea misikiti zaidi kuliko kanisa,mfano Tabata dampo katika uvunjaji wa nyumba msikiti haukuguswa na zinatumika gharama kubwa na ushirikishwaji unakuwepo" alisema Kakobe.

Pia Kokobe aliendelea kusema kuwa hayo yanayofanyika hapo Serikali haiwezi wala kuthubutu kuyafanya katika makanisa mengine hasa kwa Kardinal Pengo.

"Huu ni ujinga mtupu,na kama angekuwa Kardinal Pengo asingethubutu kuuruhusu kufanyika kwake kamwe" alisema.

Alibainisha kuwa ni juzi tu Serikali imemuita yeye kuwa ni kichuguu tu hivyo anataka kuwadhihirishia kuwa hawawezi kumkanyaga vile wapendavyo na wasitarajie hilo kutokea kamwe.

Baadhi ya waumini waliokuwepo kanisani hapo wamesema kuwa wanaungana na Askofu wao ili kuhakikisha nyaya hizo hazipitishwi eneo hilo na watakuwepo kwa muda wote.

"Tupo tayari hata kuzolewa na tinga tinga lakini hawapitishi nyaya hizo hapa na tutakuwepo kwa masaa 24 na tutahakikisha hilo linatekelezeka" walisema waumini.

Muumini mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Jackson Mgesa alisema kuwa wapo kambini hapo kwa hali ya tahadhari na kuishinikiza Tanesco kutopitisha nyaya hizo kwani hazihitajiki kupitishwa eneo hilo kama walivyofanya chuo kikuu cha Dar es salaam.

source.nifahamishe.com

0 comments:

Post a Comment