Jeshi la Israel Lawafundisha Mbwa Kuwang'ata Wanaosema 'Allahu Akbar'

Wednesday, January 06, 2010 / Posted by ishak /


Kwa mujibu wa mbunge mmoja wa Israel, jeshi la Israel limewafundisha mbwa wake kuwang'ata watu wote watakaopiga kelele za 'Allahu Akbar' (Mungu Mkubwa).
Jeshi la Israel linadaiwa kuja na silaha mpya ya kupambana na waarabu wa Palestina kwa kuwafundisha mbwa wake kuwang'ata watu wanaopiga kelele za "Allahu Akbar, Allahu Akbar".

Akiongea na shirika moja la habari la nchini Israel, mbunge mmoja wa Israel mwenye asili ya kiarabu, Ahmed Tibi, alisema kuwa jeshi la Israel limewapa mafunzo baadhi ya mbwa wake kuwang'ata watu wote wanaopiga kelele za "Allahu Akbar, Allahu Akbar".

"Mbwa wa jeshi la Israel wamefundishwa kuwashambulia waarabu wote watakaopiga kelele za Allahu Akbar", alisema Mbunge huyo.

Mbunge Tibi alisisitiza kuwa ndugu wa wanajeshi walioshuhudia shoo ya jeshi la Israel iliyofanyika jumapili, walilishuhudia tukio hilo.

Madai hayo ya mbunge Tibi yanafuatia madai ya mtangazaji wa radio ya jeshi la Israel, Carmela Menashe ambaye alisema kuwa mbwa wa jeshi la Israel wamepewa mafunzo kuwashambulia waarabu wanaopiga kelele za "Allahu Akbar".

Kwa mujibu wa gazeti la Israel la Haaretz, jeshi la Israel limekanusha madai hayo ya mbunge Tibi na kusema kuwa mbwa wao hawajapewa mafunzo hayo bali wamefundishwa kuwajua adui wakiwa wamevalia unifomu zao au nguo za kiraia.


source;nifahamishe