Afariki Baada ya Kuangukiwa na Ndege

Thursday, March 18, 2010 / Posted by ishak /


Mwanaume mmoja nchini Marekani ameiaga dunia baada ya kuangukiwa na ndege ndogo ya injini moja wakati alipokuwa akitembea pembeni mwa ufukwe wa bahari.
Ndege ya injini moja imemua mwanaume aliyekuwa akifanya mazoezi ufukweni, baada ya kumuangukia wakati ilipopata hitilafu angani.

Ndege hiyo ilipata hitilafu kwenye injini yake wakati ikipaa kuelekea Virginia toka Florida.

Ndege hiyo ilitakiwa itue kwa dharura kwenye uwanja wa ndege wa South Carolina lakini ikiwa njiani ilipata tatizo jingine la kuvuja kwa mafuta ya ndege kabla ya injini yake kuzimika kabisa.

Rubani wa ndege hiyo aliamua kunusuru maisha yake na ya abiria mmoja aliyekuwa ndani ya ndege hiyo kwa kutua kwa dharura kwenye ufukwe uliopo kwenye mji huo.

Ilikuwa ni wakati huo, ndege hiyo ilipomgonga mwanaume aliyekuwa akifanya mazoezi kwenye ufukwe huo kabla ya kuserereka na kwenda kusimama kwenye maji.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo, kwakuwa injini ya ndege hiyo ilikuwa imezimika, ndege hiyo haikuwa ikitoa kelele yoyote hali ambayo ilisababisha kugongwa kwa mwanaume huyo.

Majina ya mwanaume aliyefariki na majina ya rubani wa ndege hiyo ya abiria wanne hayakupatikana mara moja.

source nifahamishe