Alitaka Mpenzi Mmoja tu, Maelfu Wajitokeza

Sunday, March 14, 2010 / Posted by ishak /


Wakati mwanafunzi wa chuo kikuu kimoja nchini China alipoweka tangazo kwenye ubao wa shule kuwa anatafuta mpenzi, alitarajia wanaume wawili watatu wangejitokeza lakini kwa mshangao wake maelfu ya wanaume wa chuo kikuu hicho walijitokeza mbele ya chumba chake.
Ilikuwa ni siku ya wasichana kwenye chuo kikuu cha sayansi na teknolojia cha mjini Chengdu nchini China. Chuo hicho kina wanaume wengi sana kuliko wanawake. Uwiano wa wanaume 25 kwa mwanamke mmoja.

Kila mwanafunzi wa kike alipewa karatasi nyeupe akitakiwa aandike chochote anachotaka na karatasi hiyo itabandikwa kwenye ubao wa matangazo wa chuo hicho.

Msichana wa mwaka wa kwanza Zhang Mengqian kwa upande wake aliandika kwenye karatasi hiyo kuwa yeye ni mrembo sana lakini hana bahati ya kupata mpenzi, alitaka mwanaume anayetaka kuwa na uhusiano naye asimame mbele ya bweni lake kati ya saa 12:30 na 12:50 ya siku ya alhamisi ambayo ilikuwa machi 11 mwaka huu na kisha aite jina lake kwa sauti. Zhang alisema atachungulia kwenye dirisha lake kumuangalia mwanaume anayemuita, kama akipendezewa naye atashuka chini.

Zhang alitarajia mwanaume mmoja au wawili wangejitokeza, lakini siku hiyo ilifika na kwa mshangao mkubwa maelfu ya wanaume walijazana mbele ya bweni lake na kuanza kuita jina lake.

Kutokana na idadi kubwa sana ya watu waliojitokeza, Zhang alishindwa hata kuchungulia chini kuwaangalia wanaume waliojitokeza na kuamua kujifungia chumbani kwake.

Wanaume hao walisubiria kwa muda bila ya matumaini ya kuonana na Zhang na hatimaye waliamua kuondoka.

source nifahamishe