Sindano Iliyomuua Michael Jackson Kupigwa Mnada

Thursday, March 18, 2010 / Posted by ishak /


Sindano ambayo iliripotiwa kuwa Michael Jackson aliitumia kujidunga dozi kubwa ya madawa yaliyopelekea kufariki kwake, itapigwa mnada na inategemewa kununuliwa kwa dola milioni 5.
Kwa mujibu wa gazeti la The Telegraph la Uingereza, sindano hiyo inapigwa mnada mjni Las Vegas ikichukuliwa kama mojawapo ya kumbukumbu muhimu za Michael Jackson.

Vyanzo vya habari vilisema kuwa sindano hiyo inatarajiwa kununuliwa kwa dola milioni tano na huenda ikapata mnunuzi wakati wa mnada mkubwa utakaofanyika juni 25 wakati wa kuadhimisha mwaka mmoja tangia alipofariki mfalme huyo wa muziki wa Pop.

Familia ya Michael Jackson inasemekana kuwa inazo taarifa za mnada wa sindano hiyo na imekasirishwa sana na mawazo ya watu wanaotaka kunufaika na kifo cha Michael Jackson.

"Hili ni mojawapo ya matukio kadhaa ya kusikitisha", alisema mdau mmoja wa familia ya Jackson.

"Sindano hiyo haihitajiki kwenye kesi ya mauaji aliyofunguliwa daktari wa Michael Jackson, Dr Murray, lakini inasikitisha kuona kuna watu wasio na utu hata kidogo", alisema mdau huyo wa familia ya Jackson ambaye hakutajwa jina lake.

Mwanaume aliyeitia mikononi sindano hiyo amekuwa akiwasiliana na wanasheria wake kuhakikisha kuwa hakuna mtu atakayejitokeza kumnyang'anya sindano hiyo wala hatakaliwa kuipiga mnada sindano hiyo.

Michael Jackson alifariki mwezi juni mwaka jana kutokana na matatizo ya moyo kufuatia tabia yake ya kutumia dozi kubwa za madawa ya kupunguza maumivu.

source nifahamishe