Aibiwa Mumewe, Aenda Mahakamani, Alipwa Fidia Dola Milioni 9

Wednesday, March 24, 2010 / Posted by ishak /


Mwanamke wa nchini Marekani aliyemfikisha mahakamani mwanamke aliyempora mumewe, ameshinda kesi aliyomfungulia mwanamke huyo kwa kumuibia mumewe na atalipwa fidia ya dola milioni 9.
Cynthia Shackelford mwenye umri wa miaka 60 aliiambia mahakama ya North Carolina kuwa aliacha kazi yake ya ualimu ili kulea watoto na kumsaidia mumewe Allan katika kuziendeleza shughuli zake za kisheria.

Kwa kutumia kipengele cha sheria ambacho huwa hakitumiki sana, Bi Cynthia alisema kuwa mumwe alikuwa ni mtu mwenye furaha na mwenye kuonyesha mapenzi kwake kabla ya bi Anne Lundquist, 49, kuuingilia uhusiano wao na kuanza uhusiano na mumewe.

Baada ya siku mbili za kuisikiliza kesi hiyo, majaji waliamuru bi Cynthia alipwe fidia ya dola milioni 9 baada ya bi Cynthia kuithibitishia mahakama jinsi mapenzi yao yalivyokuwa motomoto kabla ya Anne kuanza uhusiano na mumewe.

Mahakama ilitaka bi Cynthia alipwe fidia kwa kitendo cha mumewe kutembea nje ya ndoa yao na kumuumiza kihisia bi Cynthia.

Anne ambaye hivi sasa anaishi na Allan, alisema kuwa atakata rufaa kupinga hukumu hiyo akidai kuwa alianza uhusiano na Allan baada ya ndoa ya Allan na mkewe kuvunjika.

Jimbo la North Carolina ni miongoni mwa majimbo machache ya Marekani ambayo yanaruhusu wanandoa kuwafikisha mahakamani wenzao wanaozisaliti ndoa zao.

source nifahamishe