Akataa Zawadi ya Tsh. Bilioni 1.3

Wednesday, March 24, 2010 / Posted by ishak /


Mwanaume wa nchini Urusi ambaye anaishi maisha ya kifukara katika nyumba yake iliyojaa mende kibao, amekataa zawadi ya dola milioni moja aliyopewa baada ya kulipatia jibu fumbo la hesabu lililowashinda wataalamu wa mahesabu kwa miaka 100.
"Nimetosheka na kile nilicho nacho", alisema Dr Grigory Perelman, 44, mwanaume anayesemekana kuwa yeye ndiye Genius wa hisabati kwani yeye ndiye mtu pekee aliyefanikiwa kulifumbua fumbo la hisabati linaloitwa "Poincare Conjecture" ambalo wanahisabati wote duniani kwa kushirikiana walishindwa kulifumbua fumbo hilo lenye miaka 100.

Dr Grigory Perelman anaishi mjini Petersburg katika nyumba yake ambayo imejaa mende wengi sana kiasi cha majirani zake kutoa malalamiko kuwa mende hawaishi kuingia kwenye nyumba zao toka kwenye nyumba ya mtaalamu huyo wa hisabati.

Dr. Perelman nyumbani kwake ana meza moja, stuli moja na kitanda chenye godoro chafu lililochakaa lililoachwa na wamiliki wa nyumba hiyo ambao walikuwa walevi kupindukia ambao ndio waliomuuzia Dr.Perelman nyumba hiyo.

Pamoja na maisha anayoishi, Dr. Perelman ameikataa zawadi ya dola milioni moja aliyopewa na taasisi ya hisabati ya Marekani akisema kuwa hana shida ya pesa ametosheka na alichonacho.

Miaka minne iliyopita, Dr. Perelman alikataa kwenda kuichukua tuzo maalumu aliyotunukiwa na umoja wa kimataifa wa wanahisabati kwa kulipatia jibu swali hilo gumu la hisabati.

Wakati huo Dr. Perelman alisema "Sina shida ya pesa wala umaarufu, sitaki nionyeshwe kwa watu kama vile wanyama kwenye bustani za wanyama".

"Mimi sio shujaa wa hisabati, sijafanikiwa kwa kiasi hicho ninachoongelewa, na hivyo sitaki watu wote wawe wananiangalia mimi", alisema Dr. Perelman.

Ilikuwa ni mwaka 2002 wakati Dr. Perelman alipokuwa akifanya kazi kwenye taasisi ya utafiti wa hisabati nchini Urusi wakati alipoanza kutuma majibu kwenye internet ya fumbo la Poincare Conjecture ambalo ni miongoni mwa mafumbo saba magumu ambayo kila fumbo moja limetengewa zawadi ya dola milioni moja kwa mtu atakayelipatia jibu.

Kupatikana kwa jibu la fumbo la Poincare Conjecture kutawawezesha wanasayansi kuweza kujua umbile la ulimwengu.

Mwaka 2003 Dr. Perelman aliacha kazi kwenye taasisi hiyo ya utafiti wa hisabati na inadaiwa na marafiki zake kuwa ameachana kabisa na masuala ya hisabati.

source nifahamishe