Mnigeria Afariki Kwa Njaa Uswizi Akigoma Kurudishwa Kwao

Monday, March 22, 2010 / Posted by ishak /


Raia wa Nigeria ambaye alianzisha mgomo wa kula akipinga kurudishwa Nigeria toka Uswizi amefariki kwenye uwanja wa ndege dakika chache kabla ya kupandishwa ndege kurudishwa kwao.
Raia huyo wa Nigeria mwenye umri wa miaka 29 alikuwa kwenye mgomo wa kula kwa siku kadhaa akipinga kurudishwa kwao Nigeria.

Raia huyo wa Nigeria ambaye alikuwa miongoni mwa wahamiaji 15 toka Nigeria waliokuwa waondoshwe kinguvu kutoka Uswizi baada ya kugoma kurudi kwenye nchi zao.

Mnigeria huyo alianza kuumwa ghafla baada ya kufungwa pingu kinguvu wakati akilazimishwa kupandishwa ndege maalumu iliyoandaliwa kuwarudisha wahamiaji makwao.

Maafisa wa Uswizi walimvua pingu walizomfunga na daktari alijaribu kunusuru maisha yake lakini jitihada za0 hazikuzaa matunda na Mnigeria huyo alifariki kwenye uwanja wa ndege wa Zurich Airport.

Wanigeria wawili ambao nao walikuwa wakirudiswa Nigeria walipohojiwa na tovuti ya habari ya Swissinfo walisema kuwa polisi walikuwa wakiwafanyia vitendo ambavyo havikuwa vya kibinadamu.

"Walitufanya kama wanyama vile, walitufunga pingu mikononi, miguuni, kwenye mapaja na kiunoni. Pia walituvalisha helmet kama za mabondia, ilikuwa ni vigumu mtu kujisogeza", alisema mmoja wa Wanigeria hao.

Mnigeria aliyefariki alikuwa akiishi nchini Uswizi tangia mwaka 2005 na alikuwa akikabiliwa na kesi ya kukamatwa na madawa ya kulevya.

Safari za kuwarudisha wahamiaji makwao zimesitishwa kwa muda huku uchunguzi wa kifo cha raia huyo wa Nigeria ukifanyika.

Mwaka jana jumla ya safari 43 za kuwarudisha makwao wahamiaji zilifanyika nchini Uswizi na jumla ya wahamiaji 360 walirudishwa makwao wengi wao wakiwa ni kutoka nchi za Afrika na nchi za kusini mashariki mwa bara la ulaya.

source nifahamishe