Mtu Aliyeishi Mwaka Mzima Bila Kutumia Pesa

Monday, March 22, 2010 / Posted by ishak /


Kutana na Mark Boyle, mwanaume wa nchini Ireland ambaye aliamua kuondokana na stress za maisha ya kutafuta pesa na kuamua kuishi mwaka mzima bila kutafuta pesa wala kutumia pesa kununua kitu chochote.
Mark Boyle mwenye umri wa miaka 30, ambaye ana shahada ya masuala ya uchumi anasema kwamba kwa mzima alioishi bila kuigusa pesa ulikuwa ni mwaka wenye furaha sana katika maisha yake na hakuwa na stress yoyote ile.

Mark kwa zaidi ya miezi 12 amekuwa akiishi kwenye gari lake aina ya caravan kwahiyo halipi pesa zozote za pango la nyumba, hanunui chakula, anaandaa chakula chake mwenyewe au kula vyakula vinavyotupwa na watu wengine.

Mark anasema kwa mwaka mzima hakutumia hata senti moja na amekuwa mtu mwenye furaha sana na anatarajia kuendelea kuishi bila pesa.

Usafiri wake ni wa kwa kutumia baiskeli aliyoiokota, simu yake inapokea tu yeye hampigii mtu simu, anatumia solar-power kuchemsha maji yake ya kuoga.

Dawa ya meno anayoitumia anaitengeneza mwenyewe kwa kutumia mifupa ya samaki. Analima chakula chake mwenyewe au anaokota vyakula majalalani. Nguo anazovaa anaziokota pia majalalani.

Mark anaendesha blogu yake ambayo anaelezea maisha yake ya kila siku. Anatumia laptop inayotumia umeme wa solar-power na hupewa muda wa kutumia wireless internet kwa malipo ya kufanya kazi za shambani.

"Umekuwa ni mwaka wenye furaha sana kuliko miaka yote ya maisha yangu, na natarajia kuendelea kuishi hivi, sioni sababu ya kurudi kwenye maisha ya dunia yanayotawaliwa na pesa", alisema Mark.

"Sina stress za kuchelewa kazini, sina stress za kulipa bili za umeme, maji au gesi na sihitaji kufanya kazi ili kuendeleza maisha yangu", alisema Mark.

Hata hivyo Mark anakiri kuwa anazikosa starehe za dunia kama vile kwenda disko au baa kwani huko pesa zinahitajika wakati yeye hatafuti wala kutumia pesa.

"Badala ya kwenda baa, huwa naweka kambi na kuwasha moto nikicheza muziki au wakati mwingine huwa nazurura mitaani", alimalizia kusema Mark Boyle.

source nifahamishe