Imani za Kishirikina Zapelekea Abanikwe Kichwa Chake

Monday, March 22, 2010 / Posted by ishak /Imani za kishirikina nchini Bangladesh zimepelekea wauzaji wa matofali ya kuchoma wamuue mtu na kisha kukibanika kichwa chake baada ya kuambiwa na mganga kuwa kufanya hivyo kutayafanya matofali yao yawe mekundu na hivyo kununuliwa kwa wingi.
Wafanyakazi wanne wa sehemu ya kutengeneza na kuuza matofali ya kuchoma nchini Bangladeshi wanashikiliwa na polisi kwa kumuua kibarua na kisha kukibanika kichwa chake kwenye jiko la kuchomea matofali.

Tukio hilo limetokea kwenye kijiji kimoja kaskazini mwa Bangladeshi baada ya mmiliki wa sehemu hiyo kuwapa maagizo wafanyakazi wake kuwa mganga ameagiza wamtoe kafara mtu mmoja ili kuyafanya matofali yao ya kuchoma yawe mekundu.

Mmiliki huyo alikuwa hana furaha na rangi ya matofali yake kutokuwa mekundu pamoja na kwamba walikuwa wakiyachoma sana matofali yao.

Matofali mekundu ni dili sana nchini Bangladeshi kutokana na kwamba watu wengi wanaamini kuwa matofali yaliyochomwa ipasavyo huwa na rangi nyekundu iliyokolea.

Wafanyakazi wa sehemu hiyo ya kutengeneza matofali walimuua mmoja wa kibarua wao na kisha kukibanika kichwa chake kwenye makaa ya moto kama mganga alivyoagiza.

Polisi wanawashikilia wafanyakazi wanne na wanamtafuta mmiliki wa sehemu hiyo pamoja na mganga wake ambao walitoroka baada ya tukio hilo kugundulika

source nifahamishe