Gaidi wa Nigeria Akifanya Mazoezi na Al-Qaeda

Sunday, May 09, 2010 / Posted by ishak /


Video imetolewa ikimuonyesha mwanafunzi wa Nigeria anayetuhumiwa kujaribu kuilipua ndege ya Marekani siku ya krismasi, akifanya mazoezi na wenzake kwenye kambi ya Al-Qaeda nchini Yemen.
Video hiyo inamuonyesha Umar Farouk Abdulmutallab na wanaume wengine wakifanya mazoezi ya kulenga shabaha kwenye kambi ya kundi la Al-Qaeda nchini Yemen linalojulikana kama "Agap".

Umar anakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kuiangusha ndege ya Marekani kwa kutumia mabomu aliyoyaficha kwenye chupi yake.

Jaribio lake lilifeli na Umar alibaki na majeraha ya kuungua na moto kwenye sehemu zake za siri.

Alikanusha madai ya kesi zote alizofunguliwa lakini shirika la ujasusi la Marekani limesema kuwa anaonyesha ushirikiano kwa maafisa wa upelelezi.

Umar mwenye umri wa miaka 23 aliwaambia wapelelezi wa Marekani kuwa alipewa mafunzo nchini Yemen. Alipewa vifaa vyenye uwezo wa kusababisha mlipuko mkubwa na kuambiwa nini anatakiwa afanye.

Umar aliwaonya Wamarekani kuwa mamia ya vijana kama yeye wapo wengi nchini Yemen wakipatiwa mafunzo na wako tayari kufanya mashambulizi wakati wowote.

Katika video iliyotolewa, Umar anaonekana akiwa ameshika bunduki na mwishoni mwa video anaonekana akitoa ujumbe katika lugha ya kiarabu.

Haijajulikana ni lini video hii ilitengenezwa na kama ni feki au la.


source nifahamishe