Watu 103 wamefariki dunia baada ya ndege ya Libya kulipuka wakati ikitua kwenye uwanja wa ndege nchini Libya huku mtoto wa miaka minane akiwa ndiye mtu pekee aliyetoka hai kwenye ajali hiyo mbaya.
Ndege ya shirika la ndege la Libya Afriqiyah Airways, iliyokuwa imebeba abiria 104 toka nchini Afrika Kusini ililipuka wakati wa kutua kwenye uwanja wa ndege wa mjini Tripoli, Libya.
Abiria wote walifariki hapo hapo lakini mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minane raia wa Uholanzi ndiye aliyenusurika maisha yake kimiujiza.
Abiria wengine 61 ambao nao walikuwa ni raia wa Uholanzi walifariki kwenye ajali hiyo
Waziri wa usafiri wa Libya, Mohamed Zidan, alisema kwamba uchunguzi unafanyika kujua chanzo cha ndege hiyo aina ya Airbus A330 kulipuka na kugawanyika vipande vipande wakati wa kutua.
"Kulikuwa na watu 104 ndani ya ndege, abiria 93 na wafanyakazi wa ndani ya ndege 11", alisema Zidan na kuongeza kuwa maiti za watu 96 zimeishatambulika.
"Kuna mtu mmoja tu aliyenusurika naye ni mtoto wa miaka minane raia wa Uholanzi ambaye anaendelea kupatiwa matibabu hospitali", alisema waziri huyo wa usafiri.
Wizara ya mambo ya nje ya Uholanzi imesema kuwa mtoto huyo amelazwa hospitalini mjini Tripoli akipatiwa matibabu baada ya mifupa yake kadhaa kuvunjika.
Tukio hili linakumbushia ajali ya ndege ya shirika la ndege la Yemen, Yemenia Airways mwaka jana ambapo mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 12, Bahia Bakari alinusurika maisha yake baada ya ndege kudondoka baharini kwenye visiwa vya Komoro na kuua watu wengine wote 152 waliokuwemo kwenye ndege hiyo.
source nifahamishe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment