Uingereza imepata waziri mkuu mpya David Cameron toka chama cha Conservative baada ya chama cha Labour kupigwa mwereka kwenye uchaguzi mkuu.
Kiongozi wa chama cha Labour, Gordon Brown alitangaza kujiuzulu jana jioni na hivyo kumaliza zengwe la uchaguzi wa Uingereza uliofanyika alhamisi ambapo hakuna chama kilichoshinda uchaguzi huo.
Vyama vikuu vitatu vya Uingereza vilishindwa kupata kura za kutosha kuwawezesha kuingia madarakani hivyo kuwepo kwa ulazima wa serikali ya mseto au ufanyike uchaguzi mwingine kama wote wakishindwa kuafikiana.
Hatimaye chama cha Liberal Democrats kilichoshika nafasi ya tatu kwa wingi wa viti bungeni kilifanikiwa kuafikiana na chama cha Conservative kilichoshika nafasi ya kwanza na hivyo kuunda serikali ya mseto ambayo inaing'oa serikali ya Labour iliyokaa madarakani kwa miaka 13.
David Cameron, mwenye umri wa miaka 43, alienda kwanza kukutana na malkia wa Uingereza kwenye jumba lake la Buckingham Palace na kupewa rasmi pendekezo la kuunda serikali.
Katika serikali ya mseto iliyoundwa, Cameron amewapa chama cha Liberal nafasi tano za uwaziri wakati kiongozi wa chama cha Liberal Democrats, Nick Clegg ndiye atakayekuwa naibu waziri mkuu.
source nifahamishe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment