Madaktari Wapagawishwa na Mtu Ambaye Hajala Miaka 70

Tuesday, May 11, 2010 / Posted by ishak /


Madaktari wa jeshi la India wameshindwa kuamini macho yao baada ya babu Prahlad Jani ambaye anadai hajala chakula kwa miaka 70, alipomaliza siku 15 walizomweka chini ya ulinzi mkali bila kula wala kunywa chochote wala kwenda chooni.
Madaktari na wanasayansi duniani wamekiri kuwa hawajui ni kitu gani kinamwezesha babu Prahlad Jani mwenye umri wa miaka 82, aweze kuishi siku nyingi bila kula wala kunywa chochote na bila kwenda haja.

Babu Jani aliwekwa kwenye chumba chenye kamera za ulinzi kibao akifuatiliwa kila anapokwenda kwa masaa yote 24 kwa siku zote 15 ambazo wanasayansi waliona zinatosha kuthibitisha kama ni kweli madai ya babu Jani kuwa hajala chakula chochote kwa miaka 70 sasa.

Madaktari wamethibitisha kuwa kwa siku 15 ambazo wamekuwa wakimfanyia uchunguzi babu Jani hajala chakula chochote wala kunywa kinywaji cha aina yoyote kile.

Babu Jani ni mfuasi wa mungu wa kihindi Amba ambaye Jani anaamini ndiye aliyempa nguvu zote hizo alizo nazo za kuweza kuishi miaka mingi bila kula wala kunywa chochote.

Kitu ambacho madaktari wanashindwa kukielewa ni jinsi Jani alivyoweza kuishi siku zote hizo bila ya kwenda haja.

Afya ya Jani ilipofanyiwa uchunguzi imeonyesha kuwa babu Jani ni mtu mwenye afya njema kuliko hata baadhi ya watu wenye nusu ya umri wake.

Jani hana matatizo ya akili na ubongo wake umeonekana kuchapa kazi kama kijana wa miaka 25.

Akiongea baada ya kutoka hospitali, Jani alitamba mbele ya waandishi wa habari kwa kusema "Niko fiti na mwenye nguvu leo mpaka madaktari wamekubali, wamenifanyia kila aina ya vipimo wanavyovijua kwa siku zote 15 na wamethibitisha kuwa sihitaji chakula ili kuishi".

"Nina nguvu na mwenye afya kwakuwa mungu ndivyo alivyotaka niwe", alisema Jani.

Madaktari wa India wanaamini kuwa jibu la kitu gani kinachomwezesha Jani kuishi siku nyingi bila kula, litawawezesha wanasayansi kubuni njia za kuokoa watu kwenye majanga ya asili kama vile matetemeko ya ardhi.

source nifahamishe