Kidedea: Kikundi cha sanaa kilichoweka mapenzi pembeni na kufanya kazi

Saturday, February 13, 2010 / Posted by ishak /


KWA wapenzi wa sanaa ya maigizo bila shaka wanaweza kuyakumbuka majina kama Peace ambaye kwa sasa ni marehemu, Jengua na mengine kadhaa yaliyokuwa yakiunda kikundi maarufu cha Kidedea, kikundi hicho kimerudi tena upya kikiwa na wasanii zaidi ya 50.
Kikundi hicho kilipata umaarufu wake kupitia michezo ya kuigiza kwenye televisheni kiasi cha wasanii wa kikundi hicho kupata kero kubwa wanapofanya shuguli zao za kawaida mitaani au wanapokuwa katika matembezi ya kawaida.

Hata hivyo umaarufu wa kikundi hicho ulizimika ghafla katikati ya miaka ya 2000 baada ya wasanii wa kikundi hicho kusambaratika na kuunda vikundi vingine vidogo vilivyokosa msisimko.

Hatimaye hii leo tunakizungumzia kikundi hicho kikiwa hai, kufuatia juhudi kubwa za mlezi na mdhamini wake wa sasa Dk Karim Kihiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa kituo cha tiba asilia zilizotafitiwa kisasa cha The Modern Traditonal Clinic.

Kwa sasa kikundi hicho kimepiga maskani yake katika ukumbi wa CCM Manzese Tip Top kikifanya mazoezi makali huku kikiwa na wasanii wasiopungua 58 wanaofanya maonyesho yote yanayohusu sanaa.

Tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo kikundi hicho kiliegemea sana katika sanaa za maonyesho kwa kufanya kazi kwenye vituo vya televisheni pekee, hivi sasa sanaa katika kikundi hicho kimegawanyika katika sehemu kuu tatu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo ndani ya Kikundi hicho cha Kidedea sasa kuna kitengo cha muziki wa asili ambapo ngoma za makabila mbalimbali ya ndani na nje ya nchi hutumbuizwa kwa umahiri mkubwa.

Vilevile muziki wa dansi kutoka karibuni pande zote za dunia likiwemo Bara Hindi hutumbuizwa kwa kupigwa 'Live' na hata kuchezwa na wasanii wa kikundi hico wanaoonekana kuiva haswa katika fani ya sanaa.

Kwa leo hii utakapopata bahati ya kuingia katika ukumbi wa CCM Manzese Tip Top na ukiwakuta wasanii wakiwa mazoezini utaamini kwamba hivi sasa wamedhamiria kuingia kwenye sanaa kwa nguvu zote.

"Kidedea" ni neno linalotamkwa na kiongozi wa kikundi hicho ambapo baadae wasanii hujibu kwa pamoja na kwa sauti kuu maneno haya.

"Kanyage twende, tunapendana bila kutakana, hapa ni kazi tu mapenzi kwenu'

Maneno haya hayatamkwi kwa mzaha, bali wasanii wanapoapa kipo hiki huonyesha dhamira kutoka mioyoni mwao huku baadhi yao wakionyesha ishara ya kugangamaa kwa kutumia miguu, mikono na hata vichwa ili kukipa nguvu kiapo chao.

Dk Karim Kihiyo katika mahojiano na Nifahamishe alisema kwamba muundo wa sasa wa kikundi cha Kidedea umelenga biashara zaidi na kumnufaisha msanii mmoja baada ya mwingine tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo faida ya msanii ilikuwa ni kuonekana kwenye luninga.

Anasema katika kuhakikisha kuwa wasanii wananufaika na kundi lao wanatumia fani mbalimbali ikiwa ni kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali ambazo zinafanyika katika jamii.

Kihiyo anasema kwa sasa wanajipanga vilivyo ili kuhakikisha kuwa kila kundi ambalo linaunda kidedea linasimama imara kwa kuhakikisha kuwa linatoa mchango wake kwa kila hali na mali.

Mkurugenzi huyo wa Kidedea anasema kuwa kwa sasa wanatarajia kutumia maonyesho mbalimbali pamoja na mabonanza ambayo yatakuwa yakifanyika sehemu za wazi kujitangaza kwa wapenzi wao.

Anasema kuwa pamoja na wao kushiriki katika mabonanza pia wataanza ya kwao wenyewe katika siku za mwisho wa wiki ambapo wanatarajia kutoa burudani ya kila aina.

"Na katika kuhakikishia kuwa tumerudi kwa kasi kubwa na matunda yetu yataanza kuoekana siku karibuni kwani kwa sasa tunajinoa vya kutosha," alisema.

Kihiyo aliweka bayana kuwa kikundi chake kimejipanga kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo zitajitokeza kwani hizo ndizo zilichangia kuyumba katika kipindi kilichopita.

Aliweka bayana kuwa mikakati yao ni kuhakikisha kuwa burudani ya asili inarudi kama ilivyokuwa hapo awali.

Anasema kuwa kundi hilo lenye wasanii 58 limezingatia vigezo mbalimbali katika kuwapata ambapo asilimia kubwa ya washiriki ni vijana.

Mkurugenzi huyo anasema pamoja na kuzingatia suala la umri pia wamejitahidi kuepuka watu ambao wanajiona kuwa ni maarufu kwani walio wengi wamekuwa wakichangia migogoro ndani ya makundi kama hayo.

"Katika kundi letu hakuna mtu ambaye atajiona yeye ni maarufu (star) wote ni sawa na hilo tutalisimamia kwani kinachohitajika hapa ni kazi mbele na mambo mengine hayana nafasi," alisema.

Alisema pamoja na kazi pia tunadumisha ushirikiano baina yetu kwani hiyo ni moja ya nguzo muhimu kwa sisi kufikia malengo ambayo tumejiwekea ambayo ni ya kila msanii kufaidika na kundi.

Alisema katika kundi hilo yupo msanii maarufu kama Mzee Kankaa lakini ameahidi kutumia uwezo wake kusaidia mafaniko ya kundi na washiriki wote kwa ujumla.

Dk. Kihiyo amewataka wadau na wapenzi wa kundi la kidedea kuunga mkono kundi hilo ambalo limedhamiria kutoa burudani ya kutosha kwa kipindi hiki na kijacho.

source nifahamishe