SIAMINI kama huyu anayezungumziwa hapa ni Rais wangu wa awamu ya tatu nchini Tanzania Benjamin William Mkapa.
Wakati huo nilikuwa najiandaa kuvuka mpaka wa Zambia na Tanzania katika mji wenye vurugu wa Tunduma mkoani Mbeya ili niweze kuingia nchi jirani ya Zambia.
Mbele yangu naona mchanganyiko wa raia wa Tanzania na Zambia wakihangaika huku na huko kujitafutia riziki, wengi wao wakiwa wafanyakazi wa magari ya mizigo.
Mji huu una pilikapilika kama zile za Manzese Jijini Dar es Salaam, lakini hauna tishio la vibaka zaidi ya watu kujitafutia maisha kutokana na shughuli wanazozifanya.
Si rahisi kupata mtu wa kuzungumza naye labda wafanyabiashara wa vyakula waliojitenga kandoni mwa kituo kikuu cha magari yatokayo kila upande.
Uzuri wa sehemu hii ya biashara hakuna anayeilaumu Serikali, wengi wanalaumiana wenyewe kwa wenyewe kwa kuzembea jambo fulani lililowakosesha kipato.
Ukivuka salama kutoka Tunduma utakaribishwa na kitongoji cha Nakonde hapa tayari utakuwa umekanyaga ardhi ya Zambia.
Hapa hakuna pilika pilika nyingi kama zile zilizokuwa Tunduma, watu wanaonekana wakihangaika na shuguli za kawaida, hata wakulima wanaweza kuonekana hapa.
"Murishani anwe" unaweza kuulizwa ikiwa ni salamu ya moja ya kabila moja la nchini Zambia.
Utakapojibu vizuri na kuulizwa nchi uliyotokea na kwa bahati nzuri ukiitaja nchi ya Tanzania hasa Jiji la Dar es Salaam utaongeza heshima kidogo.
Wataanza kudadisi kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na mengine kadhaa kuhusu Tanzania.
Humuulizia zaidi Benjamin Mkapa ambaye alipata kuwa Rais wa awamu ya tatu wa Tanzania.
"Murishani Mwapungule Mkapa?" wakiwa na maana anaendeleaje Mheshimiwa Mkapa"
Utakapojibu kwamba hajambo na sasa amejipumzisha ila bado amekuwa akishiriki na ujenzi wa taifa la Tanzania, hawatasita kumpa sifa zake alizojipatia kutokana na uongozi wake shupavu na hapo utaweza kusikia jibu hili.
Wanasema kwamba Mkapa ndiye Rais shupavu wa Tanzania ambaye anapaswa kuwekwa kwenye kumbukumbu za utendaji uliotukuka.
Wanakubali kwamba Tanzania ni moja ya nchi iliyobarikiwa na Mungu kupata viongozi bora tangu aliyekuwa muasisi wa taifa la Tanzania hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hadi Rais Kikwete ila kwa Rais mstaafu Mkapa wanazidisha sifa.
Wanamsifu Mkapa kwa namna ambayo hata raia wa Tanzania asingeweza kujua au kueleza sifa ambazo kiongozi huyo anazo.
Ukiachilia kitongoji hicho cha Nakonde utaweza kuvipitia vingine kama vile Mwenzo, Kapwila, Chozi, Chandananeyaya, na Lusiwasi, mji ambao ni makao makuu ya Jimbo la Kaskazini.
Katika vitongoji vya Mfumu, Mpika, Nkulushi River na Chambeshi wanatamani kumuona mkuu huyo wa nchi wa zamani wa Tanzania angalau aende akawatembelee.
Ukitokea Zambia unaweza ukashangazwa na kauli zinazoshabihiana katika miji mbalimbali nchini humo kuhusu sifa za Rais mstafu Mkapa, zinazotokana na uongozi shupavu uliojikita katika kukusanya kodi na kuimarisha miundombinu hasa ile ya barabara.
Wakati unapovuka mpaka wa Tanzania na Malawi ukiwa mjini Kaporo na kuelekea Kalonga maswali ya kuhusu Tanzania na uongozi wake yatazidi kuwa kero kwako.
Unaweza ukatamani usijitambulishe kuwa wewe ni Mtanzania hasa kama hutokuwa na elimu ya kutosha juu ya uraia na hatma ya nchi pamoja na mambo mbalimbali yanayoendelea nchini.
Watakapomtaja Rais Mkapa wataongeza maneno haya nanukuu: 'Sieni Mkapa akale pa pepo'
Maana yake 'mwacheni Mkapa apumzike'.
Wanalaani sana pale wanaposikia kiongozi huyo wa nchi akihusishwa na ubadhirifu.
Ukiweza kukaa katika baadhi ya hoteli zilizopo kwenye miji mikuu kama vile Blantyre au Lilongwe utapata sababu kuu za wananchi hao kumlilia Mkapa.
Kama ilivyo kwa Wazambia huorodhesha kero alizopambana nazo Mkapa katika utawala wake wa awamu ya tatu ya uongozi wa Tanzania.
"Kwanza alipata changamoto ya kwanza kabla ya kugombea Urais kwa vile hakuwa akifahamika sawa kwa Watanzania," anasema mkufunzi wa chuo cha Ualimu Usisya.
"Lakini pia alizuia mfumuko wa bei hadi anaondoka madarakani tulikuwa tumewazidi kwa bei ya vyakula kama vile mchele, unga na hata mafuta huyu aliwawezesha watu wenye kipato cha chini kufurahia maisha," anasema Mwalimu huyo.
Lakini Rais Mkapa anasifiwa kwamba licha ya kumudu kudhibiti mfumuko wa bei lakini ndiye aliyewawezesha Watanzania kupata elimu kuhusiana na uanzishaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES).
"Mpango huu umeifanya Tanzania itukimbilie kwa kiwango cha elimu, hapo zamani tuliwazidi kabisa," anaongea msomi Alex Chingalaba kutoka mji wa Lumph.
Uthamani wa Rais mstafau Mkapa kwa wananchi wa nchi jirani ni sawa na ungo ingawa hapa nchini thamani yake kwa baadhi ya watu ni sawa na uongo uliochakaa ambao katika baadhi ya maeneo hapa nchini hujulikana kama Kibeku.
Na pindi utakapoaga kutoka kwenye vijiwe hivyo wananchi hao wan chi jirani watakusisitiza kwamba "Nyie Wabongo...Sieni Mkapa".
source nifahamishe
Mkapa ni Sawa na Ungo Kwa Majirani, Kibeku Kwa Watanzania
Thursday, February 11, 2010
/
Posted by
ishak
/
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment