Nyie Njooni tu Mjini' - Mwana FA

Saturday, July 24, 2010 / Posted by ishak /


MSANII Hamisi Mwinjuma 'Mwana FA' amesema kuwa wimbo wao wa Usije mjini aliyouimba na swahiba wake Ambwene Yesaya 'Ay', haukulenga kuwaogopesha watu kuja mjini isipokuwa unawapa watu taswira halisi ya maisha ya mjini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Mwana FA alisema kuwa walipata wazo la kutunga wimbo huo baada ya kusikiliza nyimbo nyingi za wasanii wa Tanzania ambazo zinaelezea zaidi mambo ya party hali ambayo inawajengea taswira watu walioko vijijini kuwa maisha ya mjini ni ya raha.

"Hata ukiangalia video za wasanii wetu, utaona nyingi zinazungumzia raha na watu wanajichana kila kukicha. Sasa mtu wa kijijini akiona ama kusikia nyimbo hizo taswira inayomjia kichwani mjini kuna maisha mazuri".

"Wengine wanajikuta wanatoka mjini ambako angalau alikuwa anamudu kuendesha maisha yake na kuja kuteseka mjini. Sasa sisi tukaona kuwa kuna kila sababu ya kutoa elimu juu ya hili," alisema msanii huyo.

Akizungumzia ni wapi walipopata wazo hilo, msanii huyo alisema kuwa wazo kamili lilikuja baada ya kuona msongamano wa watu waliokuwa wanasubiri daladala eneo la Mwananyamala.

"Nakumbuka siku hiyo mimi na Ay tulikuwa kwenye matembezi yetu ya kawaida, sasa tulipofika Mwanyamala tukaona mkusanyiko wa watu wanasubiri usafiri. Tukaanza kuelezana. Wakati hali iko hivi kuna baadhi ya watu wanajipanga kukimbia vijijini na kuja mjini, wakati huku mjini watu wanateseka".

"Tukakumbuka wimbo wa jamaa fulani kutoka Kenya wanajiita Sauti Soul ambao wanazungumzia raha za maisha ya kijijini".

"Tukaona ala kama kijijini kuna raha hizi, vipi watu waendelee kuja kuteseka hapa mjini?. Tukamwaga ujumbe," alisema Mwana FA.


source nifahamishe