Mgombea ubunge wa jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, Bw. Nimrod Mkono ameanza kampeni yake ya kugombea ubunge kwa kugawa simu 800 kwa wananchi wake ili apate kupita.
Malalamiko hayo yametolewa na Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM kutoka mkoa huo Bw. Anthony Mtaka wakati akizungumza na Nifahamishe.com.
Alitoa malalamiko hayo kutokana na kauli ya hivi karibuni ya mbunge Nimrod Mkono ambaye anakitetea kiti chake cha ubunge, alipokaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akikiri kugawa simu na kuahidi kuendelea kugawa zaidi.
Katika kauli yake, mbunge huyo alisema kuwa ataendelea kugawaza zaidi, kwa madai kwamba zitawasaidia wana CCM kuwasiliana na pia kuweza kukichangia chama chao.
Akasema kuwa simu hizo ambazo tayari ametoa, zimegawiwa kwa utaratibu halali ulioelekezwa na chama chake kwa kuzikabidhi kwa viongozi wa chama ili wao ndio wazitoe kwa walengwa.
Mkono alisema kuwa lengo lake ni kugawa simu zaidi ya 800 ili zitatumike kwa kile kilichokusudiwa ambapo wana CCM waliopo vijijini wataweza kutoa fedha kidogo kuchangia Chama cha Mapinduzi.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Mkono imemsikitisha mjumbe huyo ambaye amedai kuwa jimbo la Musoma Vijijini lina matatizo mengi ambayo yanatakiwa kutafutiwa ufumbuzi na sio hizo simu anazogawa.
"Kauli ya mbunge wetu kwa kweli imenisikitikisha, nilisoma kwenye magazeti akikiri kugawa simu za mkononi huku akiahidi kuendelea kugawa na kuacha matatizo ya msingi jimboni mwake," alisema Bw. Mtaka.
Alisema kuwa jimbo hilo lina changamoto nyingi za maendeleo ambazo zinafanana na majimbo mengine hapa nchini, hivyo yanahitaji kutafutiwa ufumbuzi wa haraka na sio kugawa simu za mkononi.
Alidai tarafa zote za jimbo hilo zikiwemo za Kiagata, Makongoro na Nyanja zina matatizo mengi kama ubovu wa barabara, shule kukosa mabweni, vyoo na mengine mengi yanayohitaji ufumbuzi wa haraka.
"Badala ya kushughulikia hayo, mbunge anajigamba kwa kugawa simu za promosheni kwa wana CCM, hili kwa kweli mimi kama mwana CCM na kiongozi limenisikitisha sana," alisema.
Alisema kuwa ni vyema mbunge huyo akashughulikia matatizo ya jimbo badala ya hilo alilolifanya la kugawa simu eti zisaidie wana CCM kuchangia chama chao kabla ya uchaguzi.
Alisema kukichangia chama sio muhimu, lakini inategemea na mhusika yuko katika mazingira gani na kudai kuwa wananchi wa jimbo hilo wanakabaliwa na matatizo mengi yanayokwamisha maendeleo yao.
"Yeye kama mwana CCM mwenzangu, nimeona nimkumbushe hayo ili anapoendelea na utaratibu wa kugawa simu, atambue yapo matatizo ya msingi anayopaswa kuyapa kipaumbele," alisema.
Sakata la ugawaji simu hizo kwa sasa liko mikononi wa Takukuru mkoani humo ambao bado wanaendelea na uchunguzi wao ili kubaini uhalali wa mgawo wa simu hizo.
source nifahamishe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment